Katibu tawala wilaya ya Makete Joseph Chota akihutubia kwa niaba ya mkuu wa wilaya katika maadhimisho hayo
Hotuba ikiendelea.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula akitoa nasaha zake kuhusu muungano.
Wananchi wakifuatilia maadhimisho hayo
Wanafunzi wa shule ya msingi Kitula wakitoa ngonjera yao kuhusu Muungano.
Wananchi wametahadharishwa kuwa makini na makundi ama watu wanaoupinga muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwani hawana nia njema na taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Katibu tawala wilaya ya Makete Bw. Joseph Chota kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Makete katika maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyoadhimishwa kiwilaya katika Kijiji cha Kitula kata ya Kipagalo wilayani hapo.
Bw. Chota amesema wanaohitaji muungano uvunjike wengi
wao hawaangalii madhara yatakayojitokeza baadaye na badala yake wanaangalia maslahi yao na furaha ya sasa na si machungu ya baadaye.
Amesema katika muungano kwa pamoja zipo mali ambazo zimechumwa kwa pamoja hivyo muungano ukivunjwa kila mtu atagombea mali na mwishowe kutakuwa na hali ya kutoelewana hali itakayohatarisha hali ya amani ya nchi yetu.
Amesema ni vyema kila mwananchi kwa nafasi na uwezo wake akahakikisha muungano huu unadumishwa kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Bw. Francis Chaula amesema hana haja ya kuwataja wale ambao hawahitaji muungano huu uendelee kuwepo isipokuwa anaimani wananchi wa Makete ni waelewa na wameona manufaa ya muungano hivyo wataendelea kuudumisha bila kujali kelele za wachache wanaopenda Muungano huo uvunjike.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika kijiji cha Kitula kata ya Kipagalo na yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Makete yakiongozwa na kauli mbiu isemayo "utanzania wetu ni muungano wetu,tuulinde, tuuimarishe na kuudumisha".