Na
Kenneth Ngelesi
JUMLA ya kesi 21 zinazohusiana na matatizo ya wafanyakazi sehemu za
kazi, zimefunguliwa na baadhi yake kutolewa uamuzi katika Halmashauri ya
Jiji la Mbeya katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza hivi karibuni, Katibu wa Shirikisho la
Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA) mkoani Mbeya, William Mboma, alisema
kuwa kesi hizo zinahusu nia za malalamiko mbalimbali ya wafanyakazi
ikiwa ni pamoja na kuachishwa kazi kinyume cha taratibu.
Mbona alisema kuwa kati ya kesi hizo, 12 zimeshatolewa uamuzi na
wafanyakazi husika wamerejeshwa kazini kwa mujibu wa sheria katika
kipindi cha kuanzia Mei mwaka jana hadi sasa.
Hata hivyo, alisema kesi hizo zipo nyingi na zimeendelea
kushughulikiwa taratibu kutokana na upungufu wa watumishi waliopo katika
mamlaka zinazoshughulikia kesi hizo ambazo ni Mahakama Kuu Divisheni ya
Kazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini lina vyama 13
wanachama, ingawa si kila chama kina wanachama katika kila mkoa, jambo
ambalo amesema linatokana na baadhi ya wafanyakazi kutojua umuhimu
pamoja na haki zao za kisheria juu ya vyama hivyo.
Mboma alisema moja ya sababu zinazochangia kucheleweshwa kwa kesi hizo ni upungufu wa watumishi katika mahakama hizo.
Kuhusu maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi), Mboma
alisema kitaifa itaadhimishwa jijini Dar es Salaam na kaulimbiu yake ni
‘Utawala bora utumike kutatua kero za wafanyakazi’.
