SAKATA la mauaji ya raia mmoja wilayani Lushoto, aliyeuawa kwa
kupigwa risasi na polisi, limechukua sura mpya baada ya wananchi wa
Kijiji cha Viti, Kata ya Shume kususia ujumbe wa viongozi wa dini
uliotumwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Majid Mwanga kuwaomba radhi.
Mwananchi huyo, Hamis Seif (25), aliuawa kwa kupigwa risasi na askari
sita kutoka Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Lushoto, waliovamia kijiji
hicho Oktoba 17 mwaka jana katika tukio ambalo hadi sasa limegubikwa na
utata.
Katika tukio hilo, Athuman Mgazija alijeruhiwa kwa risasi na askari
hao sehemu zake za siri baada ya kufyatuliwa risasi na askari hao.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa sababu za
kiusalama, baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji hicho wamedai kuwa
ujumbe huo wa mkuu wa wilaya ulitumwa Aprili 15 mwaka huu ukiongozwa na
Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Sheikh Abbas.
Sheikh Abbas alifuatana na msaidizi wake, Amin Abbas pamoja na
Mchungaji P. Shemdolwa wa Kanisa la KKKT Usharika wa Shume na Padri Kika
wa Parokia ya Malindi.
Wakiwa kijijini hapo, viongozi hao walifanya kikao cha ndani na
baadhi ya viongozi wa kijiji hicho wakiongozwa na mwenyekiti wao, Samwel
Shelukindo kilichokuwa na lengo la kufikisha ujumbe wa kuwataka radhi.
Mkuu wa wilaya huyo, hakukiri wala kukanusha kutuma ujumbe huo katika
kijiji hicho baada ya kushindwa kujibu maswali aliyotumiwa na mwandishi
wa habari hizi kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia simu yake ya kiganjani.
Mauaji hayo yalitokea baada ya askari kuvamia nyumba ya mwananchi
mmoja, Mohamed Hamis usiku wa saa tano wakidai kutekeleza amri ya
Mahakama ya Wilaya ya Korogwe kwa kile walichodai alipuuza wito wa
mahakama hiyo katika shauri la madai.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari za uchunguzi wilayani
hapa, umebaini kuwa pamoja na kwamba sasa imepita miezi saba tangu
kutokea kwa mauaji hayo, tukio hilo limefanywa siri na mamlaka husika,
ikiwamo kushindwa kuwawajibisha askari waliohusika na mauaji hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Diwani wa Kata ya
Shume, Rashird Kisimbo, amehoji ukimya wa polisi kutowakamata askari
hao, huku wakihamishiwa vituo vingine nje ya Wilaya ya Lushoto.
Alisema wananchi wake wataendelea kuzililia damu za wapendwa wao licha ya serikali kukaa kimya bila kuchukua hatua.
Alidai kuwa kuwahamisha vituo na kuwashusha vyeo askari hao siyo
suluhisho na haiondoi uhalisia wa tukio hilo, huku akiutupia mzigo wa
lawama uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Lushoto kwa kutoingilia kati
tukio hilo.
Mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa baada ya askari hao kuvamia
nyumba hiyo, Mohamed Hamis na watoto wake pamoja na mke wake walipiga
yowe kuomba msaada wakihisi kuvamiwa na majambazi kwani askari hao
hawakuwa na sare.
Chanzo:Tanzania daima
