MAZIKO ya mtuhumiwa wa mauaji ya watu
tisa na unyang'anyi wilayani hapa, Charles Kichune, yamesuswa na ndugu
zake. Tangu Kichune afariki dunia Februari 9 kwa ugonjwa wa pumu katika
Hospitali ya Wilaya ya Tarime, hakuna ndugu aliyefika kuchukua mwili
huo.
Kutokana na kukaa mochari kwa muda mrefu na kuharibika, Halmashauri ya Mji ililazimika kusitiri mwili huo kwa kuuzika jana.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya
Tarime, Dk Michael Nega alisema walilazimika kumzika baada ya kukaa muda
mrefu bila ndugu zake kujitokeza.
“Imetulazimu kwenda kumzika Kichune
kutokana na ndugu zake kuususia mwili mochari ya hospitali hii na
kuharibika na kutoa harufu kali,” alisema Dk Nega.
Katika hali isiyo ya kawaida Jumapili
iliyopita baada ya kufariki dunia kwa Kichune, mmoja wa wakazi wa Tarime
aliyefika kutambua mwili huo, alilia na kuupiga makofi. Mkazi huyo
ambaye jina lake halikupatikana mara moja, inadaiwa amefiwa na wajukuu
zake wawili, David Yomami na Samwel Richard, ambao wanadaiwa kuuawa na
Kichune.
Vijana hao wawili waliuawa kwa kupigwa
risasi wakati wakitengeneza gari lao lililokuwa limeharibika. Kichune
alikuwa na majina zaidi ya moja ambapo katika baadhi ya maeneo alikuwa
akitambulika kama Josephat Chacha au Charles Msongo.
Polisi inadai baada ya kukamatwa,
alikiri kuhusika na mauaji ya watu mbalimbali katika kata za Binagi,
Turwa na Kitare katika vijiji vya Mogabiri, Kenyamanyori, Nkende na
Rebu.
Kichune alikamatwa Februari 6 Tanga alikokuwa akifuatiliwa na Polisi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Baada ya kukamatwa, uchunguzi wa Polisi
ulibaini kuwa baada ya mauaji ya watu tisa, alikodi pikipiki kutoka
kijiji cha Kenyamanyori alikokuwa akiishi, hadi Musoma.
Alipofika Musoma, inadaiwa alihifadhi
bunduki aina ya SMG na risasi kadhaa kwa mshirika wake, Marwa Keryoba
maeneo ya Bweri na alipokamatwa alimtaja Keryoba kuwa ndiye anayetunza
silaha hiyo. Februari 7, Polisi walifuatilia silaha hiyo kwa Marwa na
kumkuta mtuhumiwa, ambaye alitakiwa kujisalimisha lakini alikaidi na
kuwarushia risasi askari.
“Marwa aliuawa Februari 7 alfajiri
maeneo ya Bweri mjini Musoma, alipotakiwa kujisalimisha na kukaidi na
kuanza kurushiana risasi na askari," alisema Kamanda Kamugisha.
>>>HABARILEO