CHADEMA YATOA MAELEZO KUUMIZWA KWA MWENYEKITI WA CHAMA HICHO WILAYA YA TEMEKE, JOSEPHAT YONA PATRICK

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa mshtuko taarifa za  tukio la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya  ya Temeke, Josephat Yona Patrick.

Chama kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano, mbali ya kukemea kwa nguvu zote tukio hilo la kihuni na mengine ya namna hiyo yenye lengo ya ukatili dhidi ya binadamu, katika hatua ya sasa kinapenda kusema yafuatayo juu ya tukio hilo ovu ;


1. Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi juu ya tukio hilo la kutekwa na 
kuteswa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke ili ukweli ujulikane  na haki itendeke, kwa sheria kuchukua mkondo wake.

2. Chama 
kinawataka wanachama na Watanzania kwa ujumla kutulia, hasa pale ambapo  watu wenye hila na malengo yao, wanaanza kukihusisha chama na tukio  hilo. Watambue kuwa pamoja na mtu yeyote kuwa kiongozi wa chama, bado  anayo maisha yake na uhusiano na watu wengine katika jamii.

3. 
Jeshi la Polisi linapaswa kuyachukulia uzito mkubwa na unaostahili  matukio ya namna hii ambayo yanaanza kuota mizizi kutokana na watu waovu wanayoyatekeleza kutochukuliwa hatua za kisheria ambazo zingesaidia  kuzuia yasitokee tena.

4. Watanzania bado wanakumbuka kwamba 
hadi sasa Jeshi la Polisi limeshindwa kutoa taarifa za kina na kuchukua  hatua za kisheria ambazo zingesaidia ukweli kujulikana na haki kutendeka katika matukio ya kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari Dk.  Steven Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.  Hivyo ingesaidia kuzuia matukio mengine kutokea.

5. Ni kutokana
  na jeshi hilo kushindwa kuwajibika ipasavyo katika matukio mengine ya  namna hiyo, watu waovu wanaweza kutumia mwanya wa kinachoendelea ndani  ya CHADEMA kwa chama kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wanachama  wasio waadilifu, kufanya matukio ya namna hiyo iii kujenga taswira ya  kukihusisha chama na uhuni huo unaobeba kila sifa ya kuitwa ukatili  dhidi ya binadamu.

6. Aidha kushindwa kwa Jeshi la Polisi 
kuwajibika ipasavyo katika kufanya uchunguzi wa matukio hayo  (yaliyotolewa kama mfano hapo juu) na mengine ya namna hiyo, jeshi hilo  linazidi kujiweka katika wakati mgumu wa kukwepa tuhuma za baadhi ya  watendaji wake kujua na kushiriki masuala haya, hususan kwa kurejea  tukio la kutekwa kwa Dkt. Ulimboka.

Imetolewa leo Jumanne, Januari 7, 2014 na;

Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo