RAIS KIKWETE AKUTANA WAZIRI WA NISHATI NA MIGODI WA ALGERIA LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Januari 7, 2014, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati na  Migodi  wa Algeria Mheshimiwa  Youcef Yousfi ambaye yuko katika ziara ya siku sita nchini.
Katika ziara hii, Mheshimiwa Yousfi na ujumbe wake unaojumuisha viongozi wa mashirika ya umma, wanatarajia kutembelea kituo cha umeme cha Gridi ya Taifa cha Ubungo mjini Dar es Salaam, ujenzi wa bomba la gesi katika eneo la Vikindu na Mkuranga mkoani Pwani, machimbo ya Mererani  na Minjingu mkoani Manyara.
Rais Kikwete ameeleza kufurahishwa kwake na ziara hiyo, akisisitiza kwamba Tanzania na Algeria zimekuwa marafiki na washirikia wa karibu wa siku nyingi katika masuala ya siasa na uchumi, kufuatia  misingi imara iliyowekwa na waasisi wa nchi hizo - Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mheshimiwa Ahmed Ben Bella,
Rais amebainisha kwamba ushirikiano wa nchi hizi mbili  ni muhimu sana sio tu katika kuendeleza uhusiano wao wa  muda mrefu, bali pia katika  uwekezaji na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu.
Alisema Rais: "Tunahitaji washirika wazoefu, waaminifu na wenye ujuzi katika sekta ya mafuta na gesi kama Algeria katika kuendeleza sekta hiyo ambayo ni mpya kwetu”.
Alitolea mfano wa uzoefu wa miaka mingi wa Algeria katika uchimbaji na usafirishaji wa gesi asilia katika mradi wa bomba la gesi la Maghreb–Europe, unaounganisha machimbo ya gesi ya Hassi R'Mel nchini Algeria, na kusafirisha gesi asilia hadi nchi za Morocco, Hispania na Ureno
"Tanzania itanufaika sana na juzi na uzoefu wa Algeria katika sekta ya gesi hasa katika wakati huu ambapo Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC) limepewa jukumu la kujiendesha kibiashara hivyo linahitaji washirika mahiri", alisema Rais

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM

07 Januari, 2014


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo