WATUHUMIWA WA SHAMBULIO LA WESTGATE WANYIMWA DHAMANA

Wanaume wanne wanaoshukiwa kuhusika katika shambulio la Westgate wakiwa kortini Nairobi Novemba 4, 2013. Picha/PAUL WAWERU 
Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA wanne wa ugaidi wanaohusishwa na shambulizi la duka la Westgate Septemba 21 ambapo watu 67 walikufa Jumatano walinyimwa dhamana.

Hakimu  mkuu katika mahakama ya milimani Nairobi Bw Kiarie Waweru Kiarie alisema “washukiwa hao ni hatari na wakiachiliwa watatoroka.”

Bw Kiarie aliamuru serikali iwasilishe ushahidi katika kesi hiyo ndipo washukiwa wajue hatma yao.

“Nakubaliana na upande wa mashtaka kwamba kesi inayowakabili washtakiwa ni mbaya na adhabu yake ni kali. Wakiachiliwa kwa dhamana wakati huu huenda wasifike kortini tena wakati wa kusikizwa kwa kesi,”akasema Bw Kiarie.

Alikubaliana na wakili wa Serikali  Bw Warui Mungai kwamba “ baadhi ya washtakiwa hao hawana makao maalum na wakiachiliwa mahakama haijui kule inaweza kuwapata wakikosa kufika kortini.”

Bw Kiarie aliamuru kesi hiyo ianze kusikizwa Desemba 19, 2013.

Bw Warui alikuwa amepinga ombi la washukiwa hao  Mabw  Mohammed Ahmed Abdi, Liban Abdullahi Omar, Adan Mohammed na Hussein Hassan Mustafah.

Wakili Mbugua Mureithi anayewawakilisha washukiwa hao alimsihi hakimu mkuu katika Mahakama ya Milimani Nairobi Waweru Kiarie Waweru , “ apewe muda wa siku nane ndipo ajibu madai ya kiongozi wa mashtaka Warui Mungai kwamba washukiwa hao watatoweka wakiachiliwa kwa dhamana.”

Bw Mureithi alimweleza hakimu kwamba atawasilisha taarifa ya kiapo akisimulia yaliyowafika washukiwa hao wakiwa korokoroni pamoja na “ masuala mengine muhimu ya kisheria.”

Wakili huyo alisema anahitaji muda ndipo ajibu kila adai dhidi ya wateja wake kwa “ vile haki zao zimevunjwa.”
Bw Muriethi alisema “ hakupata muda wa kutosha kuwasiliana na jamaa za washtakiwa ndipo apate taarifa kamili kuwahusu.”

Alisema atamkabidhi Bw Mungai nakala ya taarifa atakayowasilisha kortini ndipo aijibu ikiwa atakuwa na jambo la kusema.

Wakili huyo wa serikali (mungai ) alimweleza hakimu kwamba anahitaji muda wa siku nne kujibu masuala ambayo yatasemwa na Mabw Abdi, Omar, Mohammed na Mustafah.

Shtaka
Wanne hao wanakabiliwa na shtaka la kushambulia duka la Westgate wakishirikiana na magaidi wengine wa kundi la Al Shabaab mnamo Septemba 21, 2013 ambapo watu zaidi ya 60 walikufa na wengi wakajeruhiwa.

Pia washtakiwa hao wanadaiwa  waliwaunga mkono magaidi Mohammed Abdinur Said, Hassan Mohammed Dhohullow na wengine kutekeleza tendo la ugaidi kwa kusababisha maafa katika duka la Westgate.

Mshukiwa Mohammed Ibrahim anakabiliwa na shtaka la kumpa makao Abdikadir Hared Mohammed ajulikanaye kwa jina jingine  Mohammed Hussein akijua ametekeleza tendo la ugaidi mnamo Oktoba 7.

Adan Mohammed Ibrahim anakabiliwa na shtaka la kujiandikisha kama raia wa Kenya ilhali ni raia wa Somalia. Anashtakiwa alijiandikisha katika kaunti ya Mandera mnamo Julai 13, 2013.

Bw Ibrahim anakabiliwa na shtaka la kupatikana nchini Kenya bila hati za kumwezesha kukaa nchini Kenya ilhali ni raia wa Somalia.

Alikutwa na maafisa wa idara ya uhamiaji katika Madrasa ya Salman Al-Faris katika mtaa wa Eastleigh Nairobi mnamo Oktoba 14,2013.

Bw Hussein Hassan Mustafa anakabiliwa na shtaka la  kuwahifadhi magaidi Hassan Mohammed Dhohullow na Mohammed Abdinur mnamo Septemba 21, 2013. Amekana aliwahifadhi magaidi hao akishirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa kortini.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo