MWANAMKE amehukumiwa jela miaka 10 kwa
kuwasilisha taarifa ya uongo katika kituo cha polisi cha Emali, Kaunti
ya Makueni kwamba alikuwa amenajisiwa.
Afisa mkuu wa
polisi wilayani Nzaui, Bw Kaburu Manyala alieleza kuwa mwanamke huyo
alifika katika kituo hicho na kudai kuwa kuna mwanamume aliyekuwa
amemnajisi.
Bw Manyala
aliamrisha maafisa wake kumpeleka mama huyo katika hospitali ya
Makindu kufanyiwa uchunguzi ambao ulithibitisha kwamba alifanyiwa
kitendo hicho.
Mahakama
ilifahamishwa kuwa mshukiwa aliyedaiwa alipokamatwa iligunduliwa kuwa,
Kalumu Munyala, 21 hakuwa amenajisiwa kama alivyodai.
Mwanamume
huyo alieleza kuwa alimtongoza mama huyo na baada ya kukubaliana
walienda na kukodisha chumba katika baa moja wakalala hadi asubuhi
na kumlipa Sh300 kabla ya kila mmoja kwenda zake.
Polisi pia walifanya uchunguzi katika lojing’i walikodaiwa kwenda ambapo mlinzi alithibitisha kuwapatia chumba.
Hatua hiyo ndiyo iliepelekea mwanamke huyo kufunguliwa mashtaka ya kutoa habari za uongo.
Onyo kali
Mwanamke huyo
alikiri shtaka mbele ya Hakimu Mkuu wa Makindu, Bw Michael Kizito kabla
ya kupokezwa kifungo cha miaka 10 jela bila faini.
Wakati huo
huo, Bw Manyala ametoa onyo kali kwa wanawake wanaozurura kituo cha
biashara cha Emali na kufanya ukahaba na kuwatapeli wanaume pesa
kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia
aliwatahadharisha wanaouza bangi, dawa za kulevya na kunyonya
mafuta ya dizeli kutoka kwenye malori ya masafa marefu.
Uchunguzi
uliofanywa hivi punde na wizara ya afya ni kwamba kituo cha
biashara cha Emali ni miongoni mwa vituo vya biashara
vinavyoongoza kwa ugonjwa hatari wa Ukimwi.
