Mahakama
kuu Kanda ya Dodoma inaendelea na vikao vyake mjini Singida, imemwachia
huru kijana Elikana Selemani (28) mkazi wa kijiji cha Sefunga wilaya
ya Singida vijijini, baada ya kukiri kosa la kumuuwa Omari Muna bila
kukusudia.
Imedaiwa kuwa Elikana alitenda kosa hilo la mauaji, wakati akimuokoa mama yake mzazi asibakwe na kina Omari Muna.
Mapema
mwendesha mashitaka mwanasheria wa serikali Masanja, alidai mbele ya
Jaji Rehema Mkuye, kuwa mnamo Januari 31 mwaka jana saa 4:00 asubuhi
huko katika kijiji cha Sefunga wilaya ya Singida vijijini, mshitakiwa
Elikana alimpiga fimbo moja kichwani Omari Muna na kusababisha kifo
chake baada ya siku mbili.
Masanja
alisema siku ya tukio, mshtakiwa Elikana akiwa nyumbani kwao, alisikia
yowe kutoka kwa mama yake mzazi akiomba msaada kutoka ndani ya shamba
lao la mahindi.
Alisema
Elikana akiwa amebeba fimbo, alipofika eneo la tukio, alishuhudia Omari
Muna, akiwa amemlalia juu mama yake akitaka kumbaka.
Kabla
ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka Masanja, aliiomba
mahakama hiyo itoe adhabu kwa mshitakiwa kadri itakapoona inastahiki.
Kwa
upande wake wakili wa mshitakiwa Raymond Kimu, aliiomba mahakama hiyo,
impe mteja wake adhabu nafuu kwa kuzingatia kuwa ni kijana pekee
anayetegemewa na mama yake mzazi.
Masanja
alisema “Pia marehemu Omari amechangia kifo chake ,kwa kitendo chake
kiovu cha kutaka kumbaka mwanamke mwenye umri sawa na wa mama yake”.
Aidha, alisema mama yake pia anataka kumwona Elikana ili pengine ataacha kufikiria kitendo cha kinyama alichotaka kufanyiwa.
Akitoa
hukumu hiyo, Jaji Mkuye alisema mshitakiwa ni kijana anayetegemewa na
mama yake na vile vile toka siku ya kwanza ameendelea kutoa ushirikiano
kwa kukiri kosa la mauaji hadi mahakama kuu.
Hili jambo ni baya sana na kwa vyo vyote litamsumbua maisha yake yote.
Amesema hata mama yake Elikana tukio hilo la kuta kubaka kushuhudiwa na mtoto wake, pia litamsumbua maisha yake yote yaliyobaki.
Jaji
Mkuye amemwambia kijana huyo “Kwa hali hiyo, mahakama hii inakuachia
huru kwa sharti kwamba usitende kosa lo lote la jinai kwa kipindi cha
miezi 12”.