RAIS KIKWETE ATANGAZA KIAMA KWA MAJAMBAZI NCHINI

Amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, Rais Jakaya Kikwete ametangaza operesheni kali ya kuwasaka majambazi wanaojihusisha na uhalifu ikiwemo utekaji wa magari na wahamiaji haramu itayoanza wiki mbili zijazo na ameagiza wahusika kuanza kujisalimisha wao na silaha wanazomiliki kinyume na utaratibu.
 
Amiri jeshi mkuu Rais Jakaya Mrisho Kiwete ametoa onyo na agizo hilo wakati akiwahutubia wananchi wa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kwenye sherehe za kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kagoma Rusaunga yenye urefu wa kilomita 154 inayojengwa kwa kiwango cha lami na akafafanua kuwa operesheni hiyo itakayohusisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama itaanza wiki mbili zijazo katika mikoa ya Kagera, Geita na Kigoma na ameonya kuhusu wahalifu hao watakaothubutu kuwafyatulia risasi wanajeshi watakaokuwa kwenye operesheni hiyo.
 
Kuhusu barabara Rais Kikwete amesema serikali imedhamiria kuiunganisha miji mikuu yote ya mikoa kwa barabara za lami chini ya miradi mbalimbali ya barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami inayotekelezwa kwenye mikoa mbalimbali nchini lakini akawahimiza watanzania kuhusu umuhimu wa kuzitunza barabara hizo ili zidumu kwa miaka mingi.
 
Katika hotuba yake ya utangulizi waziri wa ujenzi Dk John Magufuli amesema barabara hiyo kutoka Kagoma Rusaunga imejengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 191 ikiwa ni fedha zinazotolewa na serikali ya Tanzania ambapo mtendaji mkuu wa Tanroads injinia Patrick Mfugale amesema kazi hiyo ambayo imeshakamilika kwa asilimia 96 inatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
 
Wakiongea kwenye mkutano huo baadhi ya mawaziri waliofuatana na rais katika ziara hiyo wamezungumzia mipango ya serikali ya kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wa wilaya ya Biharamulo ikiwemo maji, umeme na usafiri wa reli itakayopita hapo kutoka Isaka mpaka nchi za Rwanda na Burundi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo