MBUNGE
wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA), jana alishikiliwa kwa
zaidi ya saa tatu na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa tuhuma za
kumshambulia kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Warsama.
Nassari anadaiwa kufanya shambulio hilo siku ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli.
Mbunge huyo alisema aliripoti Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Arusha
jana asubuhi akiitikia wito wa Mkuu wa Tathmini na Ufuatiliaji wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamanda Issaya Mungulu.
Alisema baada ya kufika hapo alishikiliwa na Mkuu wa Upelelezi wa
Mkoa (RCO), kwa tuhuma za kushambulia watu wilayani Monduli ambapo pia
alikataa kuandika maelezo bila wanasheria wake, Mabere Marando na Tundu
Lissu.
Nassari alisema baada ya kukataa kuandika maelezo aliambiwa avue saa
na vitu vingine kwa ajili ya kupelekwa rumande lakini hata hivyo baadaye
askari walimwambia wanampeleka Monduli.
Aliongeza kuwa hata hivyo zoezi hilo halikufanyika na badala yake
walimpa fursa ya dhamana aliyoitimiza. Taarifa za polisi kutoka Ofisi ya
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO), Duwan
Nyanda, Nassari anadaiwa kumshambulia Warsama Julai 16, mwaka huu, huko
Makuyuni.
Hata hivyo jitihada za Tanzania Daima Jumapili, kuzungumza na Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas, kuzungumzia jambo hilo
hazikufanikiwa kutokana na simu zake kutokuwa na majibu.
Naye RCO Nyanda alikiri Nassari kuripoti kituoni hapo lakini akagoma kulizungumzia suala lake kwa madai si msemaji.
Tanzania Daima Jumapili lilidokezwa kuwa polisi walianza kumtafuta
Nassari wiki iliyopita na taarifa za jambo hilo zilipelekwa kwa Mkuu wa
Upelelezi Wilaya ya Arumeru.
Nassari alibainisha kuwa Julai 24, Kamishina Isaya Mungulu alimpigia
simu na kumtaka afike polisi ambapo walivyokubaliana angekwenda jana.
Source: Tanzania Daima