CHAMA cha Utabibu wa Dawa Asili (ATME) Mkoa wa Dar es Salaam,
kimepongeza hatua ya serikali kuanza kuyang’oa mabango ya waganga wa
kienyeji na kuomba ushirikiano zaidi, ili kufanikisha zoezi hilo
nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa
wiki, Mwenyekiti wa ATME Mkoa wa Dar es Salaam, Rafael Nyampiga,
alisema zoezi hilo litakapomalizika jijini Dar es Salaam, waratibu wa
ATME, viongozi wa serikali kutoka manispaa zote watakutana, ili
kujadili changamoto na hatua zaidi za kufanya kufanikisha jambo hilo.
Nyampiga alisema zoezi hilo limeanzia kwa sasa limeanzia Wilaya ya
Temeke, kubaini waganga 30 wanaofanya kazi kinyume na sheria na kusema
kuwa wanaamini kama watashirikishwa vilivyo watakamatwa wengi zaidi.
“Sisi ndio tunaishi na watu hawa na tunajua mbinu zao zote za
ufanyaji kazi kwa utapeli, lakini kama mnavyojua sisi wenyewe au
serikali yenyewe haiwezi kufanikiwa bila ushirikishwaji wa karibu wa
pande zote mbili,”alisema.
Katika hatua nyingine, alikiri baadhi ya namba zinazowekwa kwenye
mabango huwa hazipatikani, lakini kwa kutumia wateja wao waganga
wanaofanya kazi kwa utapeli ni rahisi kukamatwa.
