MKUU wa mkoa Songwe,Luteni mstaafu Chiku Galawa, ameagiza watumishi wanne wa halmashauri ya wilaya Chunya, waliogoma kuhamia wilaya ya Songwe, waatafutwe na kuchukuliwa hatua za kisheria kwani ni wahalifu kwa kutokuwepo kwenye kituo cha kazi.
Chiku alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wakuu wa Idara ya halmashauri ya wilaya ya Songwe,akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku tatu kwenye wilaya hiyo ambapo alitembelea kata mbalimbali,kukagua miradi ya maendeleo na pia kufanya mikutano ya hadhara.
Aliwataja watumishi hao kuwa ni Ofisa Uhasibu, Andendekisye Mwaisanila, Ofisa Takwimu, Fredy Mwangalaba, Ofisa Muhifadhi Wanyama Pori,Siphrone Kavishe na Ofisa Utamaduni na Michezo,Elisha Mwakabana.
Alisema watumishi hao hawajulikani kama wanaendelea kufanya kazi katika kituo cha zamanikwa utaratibu upi licha ya kutakiwa kuhamia Songwe muda mrefu lakini hawajaripoti mpaka sasa.
Aliongeza kuwa watumishi hao ni lazima warudishwe wilayani Songwe,ili waweze kujibu tuhuma zao za uharifu,kwa kukataa kuhamia wilayani humo na badala yake wanaendelea kufanya kazi wilayani Chunya.
Chiku alisema mara watakaporudishwa wilayani humo,isiishie hapo tu bali wafikishwe pia mahakamani kwa kukataa kutii amri halali ya serikali ya kuhamishiwa kituo kipya cha kazi,ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wa aina hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa huku akionyesha wazi kuchukizwa na kitendo cha watumishi hao kugoma kuhamia Songwe,alisema serikali inaongozwa kwa taratibu,Kanuni na Sheria hivyo ni lazima watumishi hao wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Awali,Ofisa Utumishi wa wilaya ya Songwe,Benedictor Polycap,alisema wilaya hiyo mpya inakabiriwa na upungufu mkubwa wa watumishi,huku wakiwemo watumishi wanne waliogoma kuhamia wilayani humo na wanaendelea kufanya kazi kwenye wilaya mama ya Chunya,iliyopo mkoa wa Mbeya.
Alisema hatua za awali Halmashauri imesimamisha mishahara ya Watumishi hao kwani kuendelea kupokea mshahara bila kuwepo kwenye kituo cha kazi ni uvunjifu wa kanuni na sheria za utumishi wa umma.
Polycap aliongeza halmashauri hiyo inatarajia kuajiri watumishi wapya 545 ambao wamelengwa kugawanywa kwenye sekta muhimu ikiwemo ile ya afya ambazo zina upungufu mkubwa.
Kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa halmashauri pia kilihudhuriwa na Mkuu wa wilaya hiyo,Samwel Jeremiah na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Songwe,Ibrahim Sambila.
