Mkazi
wa Mji Mpya, mjini hapa Charles Kanyemba (30), ameuza redio yake ili
kumwezesha kupata fedha za kugharimia mavazi, pete ya harusi na kufunga
ndoa na Honoratha Juma (28).
Bwana
harusi huyo aliuza redio hiyo kwa Sh 70,000 baada ya kukosa chanzo
kingine cha fedha za kumwezesha kutimiza lengo lake la kufunga ndoa
baada ya kuishi uchumba kwa miaka 11.
Hivyo
alitumia fursa ya msamaha kwa wachumba sugu uliotolewa na Kanisa
Katoliki Jimbo la Morogoro kwenye jumuiya zake ambapo Kanyemba alifunga
ndoa hiyo Juni 8, siku ya sherehe ya Jumuiya ya Mtakatifu Boniface,
Mji Mpya.
Akizungumza
na mwandishi juzi nyumbani kwake Mji Mpya, Kanyemba alisema aliuza
redio ili kupata fedha za kununua mahitaji muhimu yakiwamo mavazi ya
siku ya ndoa baada ya kukaa uchumba na mkewe huyo kuanzia mwaka 2002.
“Baada
ya msamaha huo kwa wachumba sugu na ubatizo wa watoto waliozaliwa nje
ya ndoa, nilikwenda kuandikisha na ndoa ikatangazwa katika Kanisa Kuu
Katoliki la Mtakatifu Patrice kwa majuma matatu kulingana na utaratibu
wa Kanisa,” alisema Kanyemba.
Alisema ndoa yake ilifungishwa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrice, Padri Fidelis Mwesongo.
“Licha
ya kutangaziwa msamaha kwa wachumba sugu ... ni mimi pekee katika
kata ya Mji Mpya niliyejitokeza kujiandikisha na kufunga ndoa,” alisema
Kanyemba.
“Nilichukua
uamuzi kutokana na kuishi muda mrefu na kuzaa watoto wawili, hakukuwa
na haja ya kujitumbukiza katika gharama kubwa ...jambo la msingi ni
kufunga ndoa na si kuangalia gharama za harusi,” alisema.
Hata
hivyo, alisema hakuwa na fedha za kukodi ukumbi, matarumbeta siku ya
ndoa kwenye kigango cha Jumuiya hiyo kilichoko umbali wa meta 100 kutoka
nyumba wanamopanga.
Alisema
baada ya kufunga ndoa, shangazi yake aliyemtaja kwa jina la Mwalimu
Paula Jaka aliwaandalia sherehe fupi nyumbani kwake mtaa wa Kiswanya A,
kata ya Uwanja wa Taifa.
“Nilikodi
teksi kwa Sh 5,000 iliyonipeleka mimi, mke wangu na jirani yetu mmoja
kwa shangazi alikoandaa chakula; ni watu wachache sana walioshiriki
chakula na vinywaji...sherehe ilidumu kwa saa mbili tu,” alisema na
kuongeza:
“Wakati
wa kurudi nyumbani, nilirudishwa na gari la binamu yangu wa kike- mtoto
wa shangazi-namshukuru Mungu kwa kufanikisha ndoa ambayo ni tendo
muhimu kwa binadamu,“ alisema.
Hivyo alisema kutokana na umuhimu wa ndoa ndiyo sababu akauza redio, na fedha iliyopatikana alinunua nguo na vitu vingine.
“Nilidhamiria
nifunge ndoa, sikuwa na fedha ... nikawaza ni bora niuze redio yangu
nipate fedha, nikaiuza kwa Sh 70,000, nikakaa chini na kuweka bajeti ya
mahitaji muhimu hasa vitu vyangu na vya bibi harusi, viligharimu Sh
65,000,“ alisema.
Alitaja
vitu vilivyonunuliwa na gharama kwenye mabano, kuwa ni suruali ya
Jeans ya mtumba (Sh 8,000), shati la dukani (Sh 10,000) na viatu vya
mtumba (Sh 10,000).
Vingine
ni vya bibi harusi ambavyo ni gauni (Sh 10,000) na viatu (Sh 13,000),
pete mbili zilichongwa kwa sonara kwa Sh 4,000 baada ya kuyeyushwa
mkufu wa dhahabu aliokuwa nao bibi harusi ikiwa na uzito wa gramu 1.5
na Sh 5,000 zilitengwa kwa ajili ya kulipia picha tano za ukumbusho.
Hata
hivyo, alisema uvumilivu kati yake na mkewe umemwezesha kudumu kwa
miaka hiyo, kwani wakati wakianza kuishi uchumba walipanga nyumba ya
udongo eneo hilo la Mji Mpya na kulalia godoro chini na baada ya kupata
fedha kidogo, hivi sasa wamenunua baadhi ya vitu na kupanga chumba
chenye sakafu na kununua vifaa muhimu vya ndani.
"Sikuona
umuhimu wa kuliweka jambo hili la ndoa hadharani kwa ndugu
zangu...sikuwa na kianzio cha fedha...watu wanawezaje kukuchangia wakati
huna kianzio?
“Nikaona
tendo kubwa ni ndoa na kujinunulia mwenyewe na mke wangu mavazi ...hata
watoto sikuwanunulia nguo walitumia zao za zamani kwani zilikuwa bado
mpya," alisema.
Kanyemba
ambaye ni mzaliwa wa Mhonda, Turiani wilayani Mvomero, baada ya baba
yake mzazi kufariki dunia mwaka 1985 akiwa mdogo, alichukuliwa na
kulelewa na shangazi yake na kuhitimu darasa la saba mwaka 1996 shule
ya msingi Mafiga, mjini hapa.
Mwaka
1999 alihitumu mafunzo ya uchoraji katika chuo cha Tushikamane cha
Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro na mwaka 2000 alijifunza udereva
katika chuo cha Veta Kihonda na kuendesha teksi kwa muda, kabla ya
kwenda kufanya kazi kiwanda cha vifaa vya michezo cha Mazava mjini hapa
ambako aliacha kazi Februari.
Kuhusu
maisha ya baadaye, alisema anatarajia kufanya biashara ya nguo za
mitumba baada ya malipo yake kutoka NSSF kutokana na kipindi
alichofanya kazi Mazava. Mbali na kujihusisha na biashara hiyo,
alitaja shughuli nyingine kuwa ni kilimo cha nyanya nyumbani kwa mkewe
Mongwe, Mlali wilayani Mvomero.
Hivyo
alishauri vijana na watu wengine kutambua kuwa wawili wanapoamua
kufunga ndoa si gharama, bali ni hiari yao na wao wanaweza kuifanya
ndoa hiyo isiwe na gharama, tofauti na ilivyo sasa ya kujiongeza mzigo.
Honoratha
alisema ameona fahari kubwa kufunga ndoa baada ya kuishi uchumba muda
mrefu na kupata watoto wawili wa kiume. Alitaja watoto aliozaa na mumewe
kuwa ni Adriano (11) anayesoma darasa la tano shule ya Msingi Kaloleni
na Adolf mwenye umri wa zaidi ya mwaka moja.
“Tumependana,
ndiyo maana ndoa yetu tumeifunga kwa hiari yetu na kwa kiwango
tulichokuwa nacho... nimepuuza maneno ya baadhi ya wanawake wanaodai
kwenda na wakati,” alisema na kuongeza:
“Nimeshuhudia
ndoa nyingi za kifahari zinafungwa, lakini hazidumu, ndoa za watu
wanyonge na masikini ndizo zinadumu kwa kuwa wana upendo wa dhati
wakati wa shida na raha,” alisema Honoratha.
Mwanajumuiya
ya Mtakatifu Boniface, Magdalena Yohana (70) aliyezungumza na gazeti
hili baada ya kushuhudia kufungwa kwa ndoa hiyo, aliwapongeza kwa uamuzi
wa kufunga ndoa isiyokuwa na gharama za kutisha.
Hivyo
alisihi vijana na watu wengine kuiga mfano huo wakitambua kuwa ndoa ni
ya watu wawili wapendanao na kwamba ndoa za aina hiyo zinapata baraka
kubwa ya Mungu na kudumu, tofauti na zinazotumia gharama kubwa
zikiwaacha wanadoa bila kitu. Magdalena ni miongoni mwa viongozi wa
kigango hicho ambako ndoa ya Kanyemba ilifungwa, huku yeye na mumewe
Joseph Raymond (80) wakibariki miaka 57 ya maisha yao ya ndoa.