Siri za wizi uliotokea Makao Makuu ya
Polisi mkoani Mwanza zimeanza kuvuja ambapo imebainika kuwa kompyuta
aina ya laptop zilizoibwa ndani ya chumba cha vielelezo zilikuwa za
ushahidi wa kesi ya wezi wa mashine za kuchukulia fedha(ATM).
Katika wizi huo wa benki ambao ulifanyika kwenye
mashine za ATM mbalimbali na watuhumiwa watatu kunaswa Februari 10,
mwaka huu saa 6 usiku wakiiba kwenye ATM za NMB,Tawi la PPF Plaza,
Polisi walinasa vitu vingi vya watuhumiwa hao ikiwa ni pamoja na
kompyuta mbili ambazo zinadaiwa kuibwa kituoni hapo juzi.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Polisi
zimeeleza kwamba katika wizi huo uliotokea katika maghala ya Polisi,
moja kati ya vifaa vilivyoibwa ni mafaili mbalimbali ya vielelezo kadhaa
vya kesi zinazochunguzwa na polisi ikiwa ni pamoja na laptop hizo
ambazo zilikuwa ni ushahidi kwa kesi hiyo ya wizi wa ATM.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ernest Mangu
alipoulizwa kuhusiana na vielelezo vilivyoibwa Polisi, alikanusha kwamba
laptop hizo zilikuwa kielelezo cha kesi za wizi wa fedha katika ATM
lakini pia hakuwa tayari kueleza zilikuwa za kesi gani.
Wakati Kamanda huyo akikanusha baadhi ya askari
ambao wanahusika na uchunguzi huo wamedai kuwa wizi huo uliendeshwa na
maofisa wa polisi wasio waaminifu na kubainisha hakuna wizi unaoweza
kufanywa na watu kutoka nje ya polisi.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI