Mkuu wa wilaya ya Makete Bi Josephine Matiro akizungumza wakati wa kufungua rasmi mdahalo kuhusu utawala bora uliofanyika leo katika Ukumbi wa SUMASESU Tandala
Washiriki wa mdahalo huo wakimsikiliza mkuu wa wilaya wakati akifungua mdahalo huo
========
Imeelezwa kuwa maedeleo ya wilaya ya Makete yatazidi kusonga
mbele iwapo wananchi watashirikiana na viongozi waliowachagua bila woga pamoja
na wananchi kutoa maoni yao kuhusu maendeleo ya maeneo yao kwa kuwa maoni yao
ni ya msingi katika shughuli za kimaendeleo
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Makete Bi Josephine
Matiro wakati akifungua mdahalo uliofanyiaka leo katika ukumbi wa SUMASESU
Tandala ulioandaliwa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani
Makete(UMANGO) uliokuwa na lengo la kujenga tabia ya wananchi kuzungumza na
viongozi waliowachagua na kuwauliza maswali kuhusu maendeleo yao
Bi Matiro amesema endapo wananchi watashirikiana bega kwa bega
na viongozi wao kutasaidia kuharakisha shughuli za maendeleo kwa kuwa kiongozi
ana wajibu wake katika kuleta maendeleo ya eneo analoliongoza lakini pia
mwananchi naye ana wajibu wake katika hilo
“Wananchi naomba mtambue kuwa maendeleo hayawezi kutokea
kama hamtatoa mawazo yenu kwa viongozi mliowachagua na kuhudhuria midahalo kama
hii ambayo inakupa fursa ya kuuliza swali kwa kiongozi wako, endapo hutafanya
hivyo hii itasababisha malalamiko miongoni mwenu na tena mtabakia kulalamika
mitaani malalamiko ambayo hayatawafikia viongozi mnaowalaumu
Hali kadhalika katika mdahalo huo Afisa mipango Barton
Sinene kutoka halmashauri ya wilaya Makete aliwasilisha taarifa ya utekelezaji
wa mipango ya maendeleo katika kipindi cha Julai 2012-Mei 2013 katika wilaya
yake kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri bw. Iddi Nganya, ambapo
amesema kwa kipindi hiki barabara za wilaya na vijiji zimeendelea kuimarishwa
kwa kiwango cha changarawe kutoka kilomita 203 hadi kilomita 228 pamoja na
madaraja 54 ya zege yamejengwa
Amesema barabara ya Njombe-Makete imeanza kufanyiwa usanifu
lili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami ambapo utamalizika Machi 2014 pia
usanifu wa kilomita 3 unafanyika barabara ya Makete mjini na unatarajiwa
kumalizika Julai mwaka huu, zabuni itatangazwa na ujenzi wa kilomita 1.5 kwa
kiwango cha lami utaanza Agosti mwaka huu
Katika mjadala huo uliowapa fursa wananchi waliohudhuria
kuuliza maswali kwa viongozi wao, hoja mbalimbali ziliibuka na kujibiwa na
viongozi waliofika kushiriki na endapo muuliza swali hakuridhika na majibu
alipewa nafasi ya kuuliza tena swali la nyongeza
Mmoja wa washiriki aliyejitambulisha kwa jina la Atilio
Sanga ameitaka serikali kuwaambia wananchi wa kata ya Tandala kuwa ni lini
umeme utafika katani hapo na kuanza kufanya kazi kwa kuwa zoezi hilo awali
lilianza kwa kasi lakini kwa sasa haliendelei na hawafahamu ni nini
kinachoendelea kwa kuwa tangu mradi huo usimame hawajataarifiwa sababu
“Mimi ningependa serikali tuweke wazi, maana mradi huu
ulianza vizuri lakini kwa hivi sasa umesimama na hatujaambiwa kwa nini, au
mnasubiri wakati wa kuelekea uchaguzi muanze kutengeneza ili mpate kura?”
alisema Sanga
Akitoa majibu ya swali hilo Mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Makete Mh. Daniel Okoka amesema majibu ya swali hilo pia yalitolewa na
diwani wao Mh. Egnatio Mtawa wakati wa ziara ya Katibu mkuu wa CCM aliyoifanya
wilayani hapo mwezi uliopita, lakini akarudia kuwa mradi huo umesimama kutokana
na hali mbaya ya hewa kwa kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa wakati wa masika
Amesema kutokana na kunyesha kwa mvua nyingi, uletaji wa
vifaa vya kuendelea na mradi huo ulishindikana kutokana na magari makubwa ya
kubeba nguzo kushindwa kufika makete kutokana na uharibifu wa barabara, na pale
walipolzimisha kupita gari lilikwama na kuzuia mawasiliano ya barabara ya
makete-Njombe kwa siku moja
Okoka amesema wamefuatilia suala hilo na kuahidiwa kuwa mradi
huo utaendelea kujengwa kwa kasi baada ya mvua kuisha ambapo wanatarajia mwezi
huu ama mwanzoni mwa mwezi ujao mradi huo utaendelea na ujenzi hadi Tandala
Kwa upande wake mwakilishi wa idara ya maendeleo ya jamii
Bi. Jackline Mroso amesema halmashauri inatambua na kuthamini jitihada za asasi
zizizo za kiserikali za kuleta maendeleo katika wilaya ya makete kwa kuwa suala
la maendeleo ni la kushirikiana na ameyasema hayo wakatia akijibu swali
lililoulizwa na Mchungaji Adili Pagalo kutoka asasi ya ELCT Makete programu ya
pamoja tuwalee aliyeuliza kama serikali inathamini mchango wa asasi zisizo za
kiserikali
Naye mwenyekiti wa UMANGO Mchungaji Ezekiel Sanga ameuambia
mtandao huu kuwa mdahalo huo ni wa pili kufanyika wilayani hapo, ambapo
wanatarajia ndani ya mwaka huu kuendesha midahalo miwili itakayowapa pia fursa
wananchi kuchangia