WAFANYABIASHARA MAKETE MJINI WAILILIA SERIKALI KURUDISHA ADA YA LESENI ZA BIASHARA

 Afisa biashara wilaya ya Makete Edonia Mahenge akisoma barua iliyotoka wizara ya TAMISEMI iliyoagiza kuwa wakusanye ada za leseni
 Mia Kyando akichangia hoja katika mkutano huo

 Mzunguko line akichangia

 Mama Ipa Kyando akitoa hoja yake
========
Wafanyabiashara wa Makete mjini wameiomba serikali kuangalia upya na kuwapunguzia gharama za leseni mpya ambazo kwa mujibu wa sheria zinatakiwa zianze kulipiwa na wapate leseni mpya tangu Januari mosi mwaka huu

Wamesema kutokana na ugumu wa biashara na mzunguko mdogo wa hela uliopo wilayani Makete, inawawia vigumu kulipia fedha hizo ambapo wameema kutokana na hali ngumu ya maisha gharama hizo zitazidi kuwaumiza

Wakizungumza kwenye kikao kati ya Afisa biashara wilaya ya makete na wafanyabiashara hao kilichofanyika sokoni hapo, wamemtaka afisa biashara kupeleka maombi yao kwenye ngazi husika kuwa wako tayari kulipia ada ya leseni kila mwaka lakini wanaomba viwango vipungue

“Jamani hali ya wafanyabiashara hapa Makete ni ngumu, mfano mzuri tangu tumeanza kufanya kikao hapa hakuna hata mteja mmoja aliyekuja madukani mwetu kununua bidhaa, zaidi ya wanaopita ni wafanyabiashara wenzetu, sasa tutapata wapi hayo malaki ya kulipia leseni” alisema Bw. Mia Kyando

Naye Mama Kathe ambaye pia ni mfanyabiashara sokoni hapo amesema kuwa serikali imekurupuka kurudisha gharama za kulipia leseni kila mwaka kwa kuwa hivi sasa muda umekwenda na tayari wananchi wanaishi kwa bajeti na hivyo hili la sasa ni bajeti mpya ambayo itawaumiza

Akijibu hoja hizo Afisa biashara wilaya ya Makete Bw. Edonia Mahenge amesema utaratibu huo umetoka wizarani hivyo wao kama halmashauri hawana budi kutekeleza agizo hilo kama lilivyo

Amesema wanachukua mapendekezo yaliyotolewa na wafanyabiashara hao lakini wakati wanayafikisha ngazi husika, zoezi la kulipia leseni kwa mwaka huu litaendelea kama kawaida kwa kuwa wao wanatekeleza agizo la barua ya TAMISEMI mpaka hapo watakapoambiwa vinginevyo

Bw. Mahenge amesema hawatamuonea wala kumkandamiza mfanyabiashara yeyote, hivyo wafanyabiashara wote wanatakiwa kufika kwenye ofisi ya biashara wilaya ya Makete ili kuanza kulipia na kupewa leseni mpya ambazo zimeanza kutolewa tangu Januari mwaka huu, wakati ambapo wanasubiri majibu ya mapendekezo waliyoyatoa


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo