Wabunge
wanne wa Chadema, ambao waliachiwa na polisi kwa dhamana wamesimulia
mateso waliyoyapata wakiwa rumande baada ya kukamatwa juzi.
Vigogo hao;
Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi, Tundu Lissu (Singida Mashariki),
Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti maalumu), walikamatwa
juzi baada ya wao na wafuasi wa chama hicho kutawanywa kwa mabomu ya
machozi na polisi kwenye Viwanja vya Soweto, Arusha.
Wabunge hao
waliachiwa baada ya kujidhamini wenyewe huku watu wengine 65
waliokamatwa pamoja nao wakiachiwa baada ya kudhaminiwa.
Wote wanatakiwa kuripoti kwenye kituo hicho Julai 22, mwaka huu na wataelezwa hatma ya suala hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul
Chagonja alisema jeshi lake linaendelea kuwasaka Mwenyekiti wa Taifa wa
Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na kuwaonya
kuwa wanatakiwa kujisalimisha mara moja.
Chagonja
alisema Mbowe na Lema wanatafutwa kwa kosa la kufanya kusanyiko lisilo
halali katika viwanja hivyo vya Soweto walipokuwa wakitaka kuomboleza
vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally
waliofariki dunia baada ya kuumizwa kutokana na mlipuko wa bomu,
Jumamosi iliyopita.
Pia
aliwaamuru Mbowe na Lema kuwasilisha mara moja ushahidi wa kuwahusisha
polisi na shambulio la bomu na kama hawana imani na Polisi, basi
wawasilishe ushahidi wao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Lissu
Lissu,
ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
alilalamikia kitendo cha polisi kumwagia maji ya kuwasha baada ya
kumkamata.
“Walinimwagia
maji ya kuwasha kwa mfululizo nikalazimika kulala chini kifudifudi huku
nikiwa nimefunika macho kukwepa yasiingie maji. “Kuna askari walitaka
kunipiga lakini niliokolewa na mwenzao mmoja aliyenikinga
nisishambuliwe. Kwa kweli ilikuwa hali ya hatari,” alisema.
Alisema polisi hao waliomkamata walivunja miwani yake kwa makusudi akisema aliikabidhi kaunta ikiwa haijavunjika.
“Wakati
naingia mahabusu nilikabidhi miwani yangu lakini ajabu wakati tukiachiwa
ilikuwa imevunjika.” Alilalamikia hatua ya polisi kuwashambulia kwa
mabomu, kuwamwagia maji ya kuwasha walipokuwa wakiwatawanya watu
waliokusanyika Soweto akisema awali, waliwaruhusu.
“Kwa maoni
yangu na maoni ya wenzangu, hakukuwa na sababu ya polisi kupiga mabomu,
risasi na kumwagia watu maji ya kuwasha kwani ni wao ndiyo walituomba
tubebe dhamana ya uongozi kwa kwenda kuwaomba wananchi waliokusanyika
pale uwanjani kutawanyika,” alisema Lissu.
Alisema Mkuu
wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Gilles Mroto ndiye aliyewaruhusu
kuzungumza na wananchi ili watawanyike baada ya viwanja hivyo kuzuiwa
kutumika kwa shughuli ya kuaga miili ya waliopoteza maisha kwenye tukio
la bomu.
Alisema
pamoja na ruhusa hiyo, polisi waliwaruhusu Chadema kuchukua magari yao
yenye vipaza sauti ili wavitumie kuwatawanya wananchi hao lakini ajabu
polisi ikawapiga mabomu mara baada ya Arfi kuwataka wananchi watawanyike
kwenda Hospitali ya Mount Meru kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
“Kama ule
mkusanyiko haukuwa halali, kwa nini polisi haohao walikaa na wananchi
wale tangu asubuhi na wakaturuhusu kuzungumza nao ili watawanyike?”
Alisema
kisheria, mkusanyiko usio halali unastahili kusambaratishwa kwa mabomu
baada ya polisi kutoa ilani kwa wahusika kutawanyika tofauti na juzi
akisema hawakutoa ilani yoyote.
Akunaay
Akunaay
alisema polisi wanapaswa kubadilisha mbinu za kukabiliana na watu
wanaodhani wamevunja sheria badala ya kukimbilia kupiga mabomu na
kufyatua risasi.
“Mabomu na
risasi ni kukomaza watu na kuwafanya wazoee milipuko. Itafikia hatua
wananchi watajenga usugu na kuanza kupambana na polisi,” alisema na
kuongeza:
“Polisi
baada ya kutukamata na kutuweka chini ya ulinzi walitupiga hadi tukiwa
kituoni bila sababu yoyote. Nadhani askari wetu wanapaswa kuacha
kumalizia hasira zao za magumu yao yanayowakabili kwa kuwapiga
watuhumiwa.”
Mukya
Mukya
amelalamikia kitendo cha polisi kukataa kumpa fursa ya kumnyonyesha
mtoto wake mchanga akisema malaika huyo alilazimika kushinda njaa kutwa
nzima ya juzi na usiku kucha.
“Niliwaomba
polisi wanikubalie kujidhamini au wanisindikize nikamnyonyeshe mtoto
lakini walinikatalia kama vile ninakabiliwa na kesi ya mauaji,” alisema
Mukya.
Akizungumzia
suala hilo, Mwenyeki wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Susan
Lyimo alisema: “Ni kinyume cha taratibu za haki za binadamu kwa mwanamke
kunyimwa nafasi ya kunyonyesha mtoto wake.”
Polisi wajibu
Akizungumzia
malalamiko ya wabunge hao, Kamishna Chagonja alisema hakuna mtuhumiwa
ambaye anaweza kutoka mahabusu akaimwagia sifa kwa sababu siyo mahali pa
kusifiwa, bali ni mahali penye kizuizi cha muda ili kuwezesha mkondo wa
sheria kuchukua nafasi yake.
“Hatuna
(polisi), roho ya Adolph Hitler (dikteta wa zamani wa Ujerumani), tupo
kwa ajili ya kulinda wananchi na mali zao,” alisema.
Aidha,
alikanusha madai ya Mukya ya kunyimwa ruhusa ya kumnyonyesha mwanaye
akisema: “Siku hizi kuna dawati la jinsia katika vituo vyetu vya polisi
kwa hiyo kama ni kunyonyesha lazima wangesimamia utaratibu wa kumwezesha
kufanya hivyo, siyo kweli kwamba amekataliwa, haya ni maneno ya
kulichafua jeshi.”
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema wanaojihusisha na uhalifu
wowote huwa na imani kuwa watafanikiwa kujificha au kukwepa mkono wa
dola na inapotokea wamekamatwa na kuchukuliwa hatua, huanza kujitetea
kwa kuwashushia lawama polisi.
“Hasa
wanasiasa na wanaharakati wakikamatwa na kuwekwa rumande, wengi hutoa
manung’uniko mengi yakiwamo ya uongo, ilimradi kuchafua polisi mbele ya
wananchi. Hatupo kwa ajili ya kusifiwa, bali kutimiza wajibu wetu,”
alisema Sabas.
Kifo chaongezeka
Idadi ya
watu waliofariki dunia kutokana na mlipuko huo imefikia wanne baada ya
mtoto Fahad Jamal (7), aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Seliani
kufariki dunia jana. Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Paul Kisanga
alithibitisha jana kufariki kwa majeruhi huyo aliyekuwa ameumia kichwani
na kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu
(ICU).
Mmoja kuagwa leo
Kiongozi wa
Chadema, Judith Moshi aliyefariki kwenye tukio hilo la bomu, leo
anatarajiwa kuagwa kwa heshima zote za chama hicho katika moja ya
makanisa jijini Arusha baada ya polisi kukizuia chama hicho kuendesha
shughuli hiyo katika eneo la wazi.
Mkurugenzi
wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema baada ya
kuagwa, marehemu Moshi atazikwa Arusha badala ya kusafirishwa kwenda
mkoani Kilimanjaro kama ilivyokuwa imepangwa awali ili kutoa fursa kwa
wananchi wa jiji hilo kushiriki katika mazishi yake.
“Kanisa gani
na makaburi yapi tutamuagia na kumzika marehemu, tutatangaza baadaye au
kesho asubuhi baada ya mashauriano kati ya viongozi na ndugu wa
marehemu ambaye atazikwa kwa heshima zote za chama,” alisema Mnyika.
Awali,
marehemu Moshi alitarajiwa kuagwa kwenye Viwanja vya Soweto kabla ya
kusafirishwa kwenda Kilimanjaro lakini Jeshi la Polisi lilizuia shughuli
hiyo kufanyika kwenye viwanja hivyo baada ya kupokea maelekezo kutoka
kwa wamiliki wake ambao ni Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha
(AICC).
CHANZO:CHADEMA BLOG
