UONGOZI wa hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT) ya Selian jijini Arusha umekanusha vikali taarifa zilizotolewa na
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema John Mnyika kuwa serikali
ilipeleka maafisa wa usalama hospitalini hapo kwa lengo la kumdhuru
mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari pamoja na majeruhi
wa mabomu waliolazwa katika hospitali hiyo na kusema ni uzushi mtupu.
Mnyika alisema kufuatia kitendo hicho mbunge Nassari alipiga kelele
(yowe) akiwa katika korido ya wodi namba 14 aliyokua amelazwa ili kuomba
msaada baada ya maafisa hao wa usalama waliokua wamevalia mavazi ya
kitabibu na kubeba vifaa vya kitabibu kumtundikia drip aliyohisi ilikua
na lengo la kumdhuru ambayo aliitoa na kuitupa.
Mnyika alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari katika viwanja vya mahakama kuu kanda ya Arusha wakati akisubiri
wabunge wanne wa chama chake pamoja na wafuasi wao waliohusika na
mkusanyiko usio halali katika viwanja vya Soweto jijini Arusha juzi
Kwa mujibu wa Mnyika, kufuatia hali hiyo Nassari aliamua kutoroka
usiku wa kuamkia jana na kutokomea pasipojulikana ili kujinusuru maisha
yake na kwamba Chadema baada ya kupata taarifa hiyo imeamua kumtafutia
mbunge huyo hospitali nyingine itakayomtibu kwa gharama za chama hicho.
Pia Mnyika alisema mbali na tukio hilo pia polisi kwa kushirikiana na
madaktari wa hospitali hiyo wamekuwa wakiwaruhusu majeruhi wa tukio la
mlipuko wa bomu kwenda majumbani kwao kabla ya kupata naafuu ikiwa ni
hatua ya kupoteza ushahidi wa tukio hilo.
“Nassari amelazimika kutoroka hospitalini pale jana usiku baada ya
kutundikiwa drip na watu tunaowajua ni maafisa usalama waliokuwa na
lengo la kummaliza ambapo aliitoa na kisha kuanza kupiga yowe katika
korido ili kuomba msaada na alifanikiwa kutoroka sasa tutmtibu sisi
wenyewe”alisema Mnyika.
Mnyika aliwataja maofisa usalama hao kuwa John Ngowi na Flugence Mark
ambao wamekuwepo hospitalini hapo kwa siku kadhaa wakitoa huduma kwa
majeruhi wa ajali ya mlipuko wa bomu lililosababisha vifo vya watu nne
na kujeruhi zaidi ya 70.
Akijibu tuhuma hizo Kaimu mganga Mkuu wa hospitali hiyo Paul Kisanga
alisema si kweli kwamba mbunge huyo alitoroka hospitalini hapo bali
alipewa ruhusa katika hali ya kawaida baada ya kuonekana hana tatizo
lolote linalomsumbua tangu kufika hospitalini hapo.
Dk.Kisanga alisema mbunge huyo alipewa ruhusa hiyo siku ya Jumanne
majira ya saa 9.30 alasiri bila kuwa na malalamiko yoyote kuhusu kutaka
kudhuriwa na madaktari anaowadai kuwa ni maafisa usalama waliotumwa na
serikali.
Aidha alisema mbunge huyo katika kuondoka kwake hakuwa na masharti
yoyote kuwa anahitaji kupata uhamisho wa kwenda katika hospitali
nyingine yoyote kwa matibabu zaidi kwakua hata alipotembelewa na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda alimweleza wazi kuwa afya yake imeimarika.
“Mimi namshangaa Nassari kama kweli ametoa tuhuma hizo .Sisi
tumemruhusu baada ya kusema kuwa anaona afya yake imeimarika na hata
mbele ya waziri mkuu aliyasema hayo na kwanini hakuyasema hayo kwa
uongozi wa hospitali kabla huu ni uzushi”..alisema Dk.Kisanga.
Wakati huo huo, Kaimu mganga huyo alisema mtoto Fahali
Jamali(7)aliyekua melazwa katika chumba cha ungalizi maalumu(ICU)tangu
siku ya tukio amefariki dunia jana saa saba mchana kufutia hali yake
kuwa mbaya zaidi.
Dk.Kisanga alisema marehemu Fahali alifariki dunia kufuatia majeraha
makubwa kichwani yaliyosababisha matundu matatu aliyoyapata kutokana na
kulipukiwa na bomu siku ya tukio hilo.
Aliongeza kuwa mara baada ya marehemu huyo kufariki mwili wake
ulichukuliwa na jeshi la polisi pamoja na mzazi wake hadi katika
hospitali ya mkoa ya Mount Meru kwaajili ya uchunguzi zaidi kabla ya
taratibu za maziko kufanyika.
source:udakuspecially