Mke
wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama
Salma Kikwete akipokea tuzo ya Millenium Development Goals, Women
Progress Awards 2013, kutoka kwa Ms Jennie Yeung , Rais wa Shirika la
Sun Zhong Shan Foundation lililo chini ya United Nations Education,
Science, Cultural and Health Advancement Foundation la nchini
Marekani. Mama Salma alipokea tuzo hiyo baada ya kutimiza baadhi ya
malengo ya Millenia katika masuala ya ukimwi, elimu kwa watoto waliokosa
fursa na kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini Tanzania. Kulia ni
Katibu wa WAMA, Ndugu Daud Nassib na kushoto ni Dr. Judy Kuriansky,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani.
Mke
wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo Mama Salma
Kikwete akimkabidhi tuzo hiyo Katibu wa WAMA Foundation , Ndugu Daud
Nassib wakati wa kupokea tuzo hiyo huko New York nchini Marekani tarehe 13.6.2013.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akipongezwa na Dr. Judy Kuriansky, Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Columbia mara tu baada ya kukabidhiwa tuzo yake.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwahutubia waalikwa
waliohudhuria sherehe za utoaji tuzo kwa wake wa Marais wa Bara la
afrika zilizofanyika huko New York nchini Marekani. Picha na John Lukuwi
Mama Salma Kikwete akiongea baada ya kutunukiwa tuzo hiyo
======== ======== =========== ======
Na Anna Nkinda – New York
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya Malengo ya Maendeleo ya
Millenia ya mwaka 2013 kwa wanawake na Shirika la Voices of African
Mothers (VAM) la nchini Marekani kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya
kusaidia jamii wakiwemo wanawake na watoto.
Sherehe
ya kukabidhi tuzo hizo zimefanyika jana katika ukumbi wa mikutano
uliopo makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) amekabidiwa tuzo hiyo kutokana na uongozi wake
madhubuti, mafanikio na mchango wake na kujitoa kwake kuwasaidia
wanawake na watoto wa Tanzania.
Akikabidhi
tuzo hizo Nana – Fosu Randall ambaye ni Rais na mwanzilishi wa shirika
hilo alisema kuwa tathimini ilitofanyika kwa mwaka 2012 juu ya Malengo
ya Maendeleo ya Milenia wametambua kwamba malengo matatu yamefikiwa
nchini Tanzania kabla ya muda uliowekwa wa kikomo wa mwaka 2015.
Alisema kuwa wake wa Marais wa Afrika wanamajukumu mbalimbali katika
nchi zao ili kufikia Malengo hayo, Taasisi ya VAM imekuwa ikifanya
tathimini juu ya hatua zilizofikiwa na Taasisi za wake wa Marais kupitia
taarifa za mwaka na zingine zinazowasilishwa.
“Wanawake
hawa wanastahili kutuzwa kwani wamefanya kazi kubwa pamoja na kufanya
shughuli zao katika mazingira yenye changamoto nyingi ukilinganisha na
wenzao katika nchi zingine.
Hafla ya tuzo hizi siyo tu inasherehekea mafanikio ya wake wa marais wa
Afrika bali pia inawahamasisha na kuwatia moyo wakati huu ambapo mwaka
2015 unakaribia”, alisema .
Alimalizia
kwa kusema kuwa mara nyingi vyombo vya habari vimekuwa vikiandika
habari zisizokuwa sahihi kutokana na kazi zinazofanywa na wake wa
marais lakini vinasahau kuandika mambo mazuri na kazi kubwa wanayoifanya
ya kuwasaidia wananchi na kuviomba vyombo hivyo kubadilika na kuthamini
kazi kubwa wanayoifanya.
Akiongea
mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mama Kikwete alishukuru kwa tuzo
aliyopewa na kusema kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimepiga hatua
kubwa sana katika kufikia malengo ya milinia kwani vifo vya watoto
vimepungua kwa asilimia 45 na 49 kwa watoto wachanga.
Alisema
kuwa haya ni mafanikio makubwa sana japokuwa lengo ni kuondoa kabisa
vifo ambavyo vinatokana na sababu ambazo zinazuilika na katika malengo
mengine maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yanaendelea kupungua
kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2004 hadi asilimia 5.1 kwa mwaka 2011.
Mama Kikwete alisema;
“Elimu
ya msingi inatolewa bure kwa watoto wote walio na umri unaostahili na
hatua kubwa imepigwa katika kupunguza ugonjwa wa maralia na vifo vya
akina mama vinavyotokana na tatizo la uzazi”
Kwa upande wa harakati za kumkomboa mtoto wa kike alisema kuwa ni lazima
ziendelee na zizingatie changamoto mpya za mazingira mapya kwani
unapompatia elimu unampunguzia changamoto za ujinsia na kumpatia huduma
ya afya ikiwemo uzazi wa mpango, unamuwezesha kushiriki zaidi shughuli
za maendeleo ya kiuchumi, unasaidia familia yake na jamii kuweza
kuendelea.
Kwa
upande wake Dk. Judy Kuriansky ambaye ni mwakilishi wa Asasi zisizo za
Kiserikali zilizo chini ya UN alisema kuwa wake wa marais wanafanya kazi
kubwa ya kuisaidia jamii hivyo basi ni jukumu la kila mmoja kuwaunga
mkono na kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kutimiza malengo ya
maendeleo ya milinia.
Dk. Kuriansky alisema kuwa ili kufikia malengo ya milinia inatakiwa
kuimarisha miundombinu iliyopo jambo ambalo litasababisha kuifikia jamii
kwa ukaribu zaidi na kuweza kutatua changamoto zinazowakabili.
Tuzo
hizo zimetolewa kwa mara ya kwanza na shirika hilo kwa kushirikiana na
Taasisi ya The reed for Hope (RFHF) na Bethesda Counsel kwa wake wa
marais wa Afrika akiwemo Mke wa Rais wa Burundi Mama Dk. Denice
Nkurunziza, Mke wa Rais wa Equatorial Guinea Mama Constancia Mangue de
Obiang na Mke wa Rais wa Mali Mama Mintou Doucoure Epse Traore.