WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaonya baadhi ya watu wanaofanya
ushabiki wa kisiasa kwenye tukio la mlipuko wa Arusha na kuwataka
wasitumie tukio hilo kujipatia umaarufu na badala yake watumie fursa
hiyo kuwafariji walioathirika na kuwa watulivu hadi suala hilo lifikie
hatma yake.
Waziri Mkuu amesema tukio hilo ni kubwa, na kitendo hicho ni kibaya
kinachostahili kulaaniwa vikali kwa hiyo haifai watu wachahe kujipatia
umaarufu kupitia tukio hilo.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumanne, Mei 7, 2013) wakati
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwatembelea ili
kuwajulia hali majeruhi waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya
Mount Meru, jijini Arusha.
Alisema ameguswa pia na hali ya matibabu inayotolewa kwa majeruhi
katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, jijini Arusha.
Waziri Mkuu alikatisha shughuli za Bunge jana mchana na kuelekea
Arusha. Mara baada ya kuwasili KIA jana jioni, Waziri Mkuu alikwenda
moja kwa moja Parokia ya Olasiti ili kujionea hali halisi na kuwapa pole
wamunini wa Kanisa hilo.
Baadaye alikwenda kumjulia hali Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha,
Mhashamu Josephat Lebulu pamoja na Balozi wa Vatican, Mhashamu Askofu
Fransisko Padilla ambako alifanya nao mazungumzo na kuwahakikishia
viongozi hao kwamba Serikali itafanya kila iwezalo hadi iwabane
wahusika.
Akiwa hospitali ya Mount Meru leo asubuhi, Waziri Mkuu alimweleza
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti kuwa asisite kuwasiliana
na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Magesa Mulongo endapo hali ya majeruhi
itabadilika na watahitaji matibabu zaidi.
Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikabidhi vifaa vyenye thamani
ya sh. milioni 23.3 ambavyo ni dawa na vifaa tiba kwa uongozi wa
hospitali hiyo ambavyo vilitolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA) chini ya uhamasishaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kukabidhi misaada hiyo, Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu alisema jana
(Jumatatu, Mei 6, 2013), TANAPA ilitoa mablanketi 50 hospitali hiyo na
kwamba wafanyabiashara wa sekta ya utalii wa mjini Arusha wamejipanga
kutoa msaada zaidi ili kuisaidia hospitali hiyo kumudu kuwahudumia
majeruhi wa mlipuko huo.
Hadi sasa, watu watatu wamepoteza maisha kutokana na mlipuko huo
ambapo watu wanane wamekamatwa na kuhojiwa na polisi. Kati yao, wanne ni
raia wa Saudi Arabia na waliobakia ni wakazi wa Arusha. Polisi bado
wanaendelea na uchunguzi wa tulio hilo.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema
wagonjwa watatu wana hali mbaya ambapo mgonjwa mmoja yuko Muhimbili na
wawili wako hapo hapo Mount Meru.
“Watu 66 waliathirika na mlipuko huo, watatu wamefariki na kati ya
wagonjwa 63 waliobakia, wagonjwa 24 wamesharuhusiwa kurudi nyumbani,
waliobakia wanaendelea kupatiwa matibabu,” alisema.
