TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Assalaam alaykum warahmatullahi wabarakaatuh.
Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania BAKWATA, limepokea kwa
masikitiko makubwa tukio la kurushwa bomu Kanisani na kusababisha
upotevu wa maisha na majeraha kwa watu wengi wakati wa sherehe ya
uzinduzi wa jengo la Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,
Orasiti, Arusha.
Kimsingi hili ni jambo la kusikitisha, kukera na kufadhaisha
sana kutokea hapa nchini. Watanzania kwa miaka mingi, tumezoea hali ya
utulivu na amani na tukio kama hili ni changamoto kwa usalama wa
Watanzania wote nchi nzima Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania BAKWATA
linalaani kitendo hicho cha kikatili na inaviomba vyombo vya dola
kufanya jitihada zote kuhakikisha wahusika wanakamatwa na wanachukuliwa
hatua, kwani msiba huu ni wetu sote, Waislamu, Wakristo na Watanzania
wote.
Kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania mimi Sheikh
Issa Bin Shaaban Simba Mufti wa Tanzania nawapa pole wafiwa wote katika
tukio hilo na kuwaombea dua majeruhi na Mwenyezi Mungu (SW) awape tahfif
na wapone haraka na kurudi katika shughuli zao za kila siku.
Wabillahi Tawfiiq.
Wabillahi Tawfiiq.
SHEIKH ISSA BIN SHAABAN SIMBA.
MUFTI NA SHEIKH MKUU WA TANZANIA BARA.
MUFTI NA SHEIKH MKUU WA TANZANIA BARA.