Wananchi wa kijiji cha Usagatikwa kata ya Tandala wilayani
Makete wamekubali kuupokea mradi wa trekta ambalo watalazimika kuchangia kiasi
kidogo cha gharama huku serikali ikichangia kiasi kilichosalia
Hayo yamebainika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo kijijini
hapo kwa kushirikisha uongozi wa kijiji na diwani wa kata hiyo mh. Egnatio
Mtawa
Amesema endapo kijiji hicho kitapata trekta hilo litakuwa na
manufaa makubwa ikiwemo kulima mashamba yao, kusafirisha mazao, shughuli za
ujenzi ikiwemo ukarabati wa barabara pamoja na kukodishwa kwenye maeneo mengine
na kukiingizia kijiji mapato
Pamoja na hayo Diwani huyo amewasisitizia kamati ya
usimamizi wa trekta kuhakikisha inadhibiti mapato na matumizi ya trekta hilo
ili wananchi wote wanufaike na mradi huo, hivyo kuwataka wananchi hao
wakiongozwa na uongozi wa kijiji kupanga viwango vitakavyochangwa na wananchi
hao ili michango hiyo ianze kutolewa mapema
Wakitoa maoni yao wananchi hao wamesema hawaoni ugumu wa
kuchangia mradi huo, isipokuwa wanataka serikali ya kijiji kuangalia rasilimali
za kijiji walizonazo ili waziuze na kiasi kitakachosalia wananchi ndiyo
wachangie ili kuwapunguzia gharama
“Mimi sina tabu mradi huu tumeupokea kwa mikono miwili,
isipokuwa serikali ya kijiji iainishe idadi ya wananchi wa kijiji hiki tugawe
tuone kila mwananchi anatakiwa kulipia shilingi ngapi, halafu kijiji hiki kina
rasilimali kama mashamba, tuyauze na kama haitatosha kiasi kilichosalia
tuchangie sisi wananchi” alisema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la
Erick
Kauli hiyo iliungwa mkono na wananchi wote huku diwani wao
akiwatahadharisha kutouza rasilimali zote za kijiji na mwishowe kijiji kubaki
kitupu
“Wenye maamuzi ya mwisho ni ninyi wananchi, mkitaka kuuza
sawa, mkitaka kuchanga sawa, lakini hakikisheni hamuuzi kila kitu mwishowe
kijiji kinabaki kitupu watu watatushangaa” alisema Mtawa
Kijiji cha Usagatikwa ni miongoni mwa vijiji viwili
vitakavyopatiwa trekta, mradi ambao uliibiliwa na wananchi wenyewe kama njia
mojawapo ya kuwasaidia katika kilimo