Na Mariam Mkumbaru
Wakazi wa kijiji cha Ifinga katika kata ya Ifinga wilaya ya Songea mkoa
wa Ruvuma, wanakosa huduma ya vipimo vya maabara kwa kutokana na
Darubini kutumia mwanga wa jua na kipindi hiki cha mvua kifaa hicho
hakiwezi kufanya kazi.
Tobias Milinga (35) ni mtaalamu wa maabara katika zahanati ya Ifinga,
anasema kuwa kipindi cha mvua kifaa hicho hakiwezi kufanyakazi kabisa,
hivyo wagonjwa wanapatia dawa kwa jinsi anavyosema ugonjwa wake na kwa
kumuangalia kwa macho.
"Nimeanza kazi ya maabara kwa muda wa miaka 18, katika zahanati
mbalimbali lakini sijawahi kuona Darubini inatumia mwanga wa jua kama
kupima magonjwa mbalimbali, na kipindi cha mvua kama hiki huwezi
kuitumia Darubini hii,"alisema Milinga.
Milinga alisema kuwa, tatizo kubwa katika zahanati hiyo, ni kutokuwa na
umeme wa solar ambao ungeweza kutumika katika Darubini hiy0, pia
kunatatizo la maji, kifaa cha kumsafisha mjamzito mimba ikiharibika
hakuna, kifaa cha kumsafisha mtoto akinywa maji machafu baada ya
kuzaliwa hakuna pamoja na madawa ya kutibu magonjwa mbalimbali hakuna.
Milinga alisema kuwa, pia kuna tatizo la uhaba wa wahudumu katika
zahanti hii, kwa sasa tupo watumishi wawili tu, akiwemo nesi mmoja, kwa
sababu hiyo inanilazimu kuwaona wagonjwa pamoja na kuwapima magonjwa
mbalimbali kila siku.
Aidha alisema kuwa, kutokana na tatizo la uhaba wa wahudumu kwa muda
mrefu, mfanya usafi wa zahanati hii Benjamin Kalunguyeye (55) imemlazimu
kuanza kutoa huduma mbalimbali kwa wanakijiji kama tabibu.
"Nimeripoti katika zahanati hii mwezi Agosti mwaka jana 2011, nikamkuta
Kalunguyeye anatoa huduma akiwa peke yake baada wa wahudumu kukimbilia
mjini na kuacha zahanati bila ya mhudumu,"alisema Milinga.
Kwa upande wake Kalunguyeye alisema kuwa, kazi ya kuwatibu wanaifinga
amaianza mwaka 1990, kwa sasa anamiaka 22 anatoa huduma katika zahanati
hiyo kama, kungoa meno, kuzalisha, kuchoma sindano, kutoa chanjo kwa
watoto wadogo, kupima wajawazito, kusafisha vidonda na kupima magonjwa
ya maabukizi kama Gono, Kaswende na Kisonono.
"Elimu yangu ni darasa la saba lakini naipenda kazi ya utabibu na
naifanya vema kama nimesomea katika chuo cha utabibu, kitu kikubwa
kilichonisukuma kujua kazi hii, nikufuatia wahudumu kukimbia zahanati
hii na kuniachia mimi kama mfanyausafi mara kwa mara, huku nikiwaona
wanakijiji wenzangu wakipoteza maisha kwa kukosa huduma,"alisema
Kalunguyeye.
Mwaka 1985, aliajiriwa na Kanisa kama mfanya usafi katika zahanati
hiyo, hapo ndio akaanza kujifunza jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa
mbalimbali kupitia kwa waganga na manesi waliowahi kufanya kazi katika
zahanati hiyo.
Ilipofika mwaka 1989, hapo ndio akaanza kuibia ibia kutoa huduma
mbalimbali kwa wanakijiji baada ya mganga na nesi kukimbia kwa
visingizio kwamba kijiji cha Ifinga, hakuna maji safi, umeme, usafiri
pamoja na mawasiliano ya simu.
Kwa upande wake Father Roja Haule wa Kanisa Katoliki Ifinga alisema
kuwa, zahanati hiyo inamapungufu mengi yakiwemo la vifaa vya muhimu vya
kutolea huduma, madawa, umeme, maji pamoja na wahudumu wa afya, kwa sasa
kuna mtaalamu wa maabara mmoja na nesi mmoja na mfanya usafi ambaye
anatoa huduma kwa uzoefu bila ya kusomea utabibu.
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Songea Dokta Daniel Masawe, alikiri
kuwepo wa kifaa cha kupima magonjwa mbalimbali kinachotumia mwanga wa
jua, na kipindi cha mfua hakina uwezo wa kufanya kazi kabisa.
"Nafahamu uwepo wa darubini ya kupimia magonjwa mbalimbali inayotumia
mwanga wa jua, tunajipanga kwa sasa kununua kifaa kingine kinachotumia
umeme wa solar, ili kipindi cha mvua wagonjwa mbalimbali waweze kupata
huduma ya kupimwa na kutambua kinachowasumbua hususan kipindi cha mvua
kama sasa,"alisema Dokta Masawe.