Bi .Usu Mallya
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WITO: WANAWAKE
TUJITOKEZE MABARAZA YA KATIBA YA KATA/WILAYA
- Zimebaki siku tatu
Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na wanaharakati wa masuala ya haki na usawa wa Kijinsia, haki za Binadamu,
Demokrasia, Utawala bora na Maendeleo (FemAct), wanaharakati ngazi ya jamii,
washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo za kila Jumatano(GDSS) na wanachama
wa Vituo vya Taarifa na Maarifa katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Shinyanga na Pwani
tunafuatilia kwa umakini mchakato mzima wa kuandaa katiba mpya.
Kutokana na
hili, taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) Mhe.
Jaji Mstaafu Joseph Warioba, kuhusu uundwaji wa mabaraza katika ngazi ya Kata/Wilaya ina
umuhimu wa pekee katika mchakato mzima wa katiba mpya nchini Tanzania.
Kwa
mantiki hiyo Mtandao wa Jinsia Tanzania inatoa rai na shime
kwa Wanawake wote vijijini na
mijini kutumia fursa na kujitokeza kwa
wingi kujiunga na mabaraza ya Katiba zikiwa zimebaki siku tatu kufikia siku ya
mwisho ya kuwasilisha maombi.
Mabaraza ya
Katiba ni chombo muhimu, cha kujadili na kuchambua rasimu ya Katiba ambayo
itatolewa na Tume ya Katiba mwezi Mei mwaka huu. Hii ni fursa muhimu kwa wananchi
hususani wanawake kujadili, kuichambua rasimu na kuhakikisha kuwa imebeba sauti
za raia wote na maoni ya makundi yote hususan wanawake na makundi mengine
yaliyoko pembezoni.
TGNP tunawakumbusha
na kuwaasa wananchi wote hususan wanawake kuchangamkia fursa hii adimu ya
kuomba kuteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa Baraza katika ngazi ya Kata na
Wilaya kama ilivyotangazwa na Tume.
Aina za ushiriki:
- Kutokana na utaratibu uliowekwa, wanawake wote wenye sifa za kuwa wajumbe wanatakiwa kuandika barua kwa Watendaji wa Vijiji/Mitaa kuomba kuteuliwa kujiunga na baraza la Katiba kabla ya muda uliowekwa kumalizika ambao ni Machi 8 hadi 20, 2013.
·
Kwa mujibu wa Kifungu kidogo cha (6), Kifungu cha 18 cha Sheria ya mabadiliko ya Katiba, Tume
inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya watu kuandaa mikutano kwa ajili ya
kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya rasimu ya Katiba na kisha
kuwasilisha maoni hayo kwa Tume kabla ya August 14, 2013.
Tunatoa wito
kwa wanawake wote mmoja mmoja na kwa
makundi yenye uwezo kufanya hivyo kulingana na utaratibu huo. Aidha tuwape moyo
wenye uwezo miongoni mwetu wajitokeze kwa wingi.
Hata kama
tumeshawahi kutoa maoni yetu kwenye mikutano iliyotangulia, bado tunaweza
kuomba nafasi hizi, kwa vile hii sasa ni rasimu ya katiba yenyewe, na ushiriki wetu mpana kwenye
mabaraza ya kata na wilaya utatuwezesha kujadili na kuichambua kwa umakini
zaidi rasimu ya Katiba na kuhakikisha madai yetu tuliyoyawasilisha wakati Tume
ilipopita kukusanya maoni yamezingatiwa.
Tusisahau kuhakikisha masuala yenye kuzingatia
haki za kijamii yameingizwa na kuwa masuala ya kijinsia yamepewa kipaumbele. Tunataka
Katiba itakayobeba sauti na maoni yetu ikilinda maslahi ya jamii nzima bila ubaguzi
wa aina yeyote. Muda uliotolewa
kuwasilisha maombi ni Machi 8 hadi 20, 2013. Wahi sasa!
Imetolewa na
Usu Mallya
Mkurugenzi Mtendaji TGNP
