Na Frank Leonard
IKIWA imebaki takribani miezi minne mwaka wa fedha wa 2012/2013
umalizike, Ofisi ya Mratibu wa Ukimwi wa Halmahsuari ya wilaya ya Iringa
haijapata fedha yoyote kutoka katika bajeti yake na hivyo kuathiri
utekelezaji wa mipango yake.
Mratibu wa Ukimwi wa halmashauri hiyo,
Odia Hezron alisema jumla ya Sh Milioni 138 ziliidhinishwa kwa ajili ya
kazi za ofisi yake katika kipindi cha mwaka huo wa fedha.
“Hii ni changamoto kubwa kwasababu
mipango mbalimbali inayohitaji fedha utekelezaji wake unakwama japokuwa
nina imani fedha hizo zitakuja hata kama ni kwa kuchelewa,” alisema.
Alisema bajeti hiyo ni kwa ajili ya
kukabiliana na matokeo ya Ukimwi, kutoa elimu, na uratibu wa shughuli
mbalimbali za Ukimwi katika halmashauri hiyo.
Katika kukabiliana na matokeo ya
Ukimwi, Hezron alisema wajawazito, watoto yatima na wanaoishi na Virusi
Vya Ukimwi (VVU) wakiwemo watumishi wa halmshauri hiyo wamekuwa wakipata
misaada mbalimbali.
“Kwa upande wa wajawazito na watumishi
upo utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya lishe ili ziwasaidie
kuboresha afya zao na kwa upande wa watoto yatima tunao utaratibu wa
kugharamia ada za shule huku wananchi wengine wakihamasishwa kuanzisha
vikundi vya ujasiriamali na kupewa msaada,” alisema.
Alisema kwa njia ya elimu, halmashauri
hiyo imekuwa ikiendesha kampeni za kukabiliana na janga hilo kupitia
sinema, makongamano na mikutano kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
Akizungumzia maambukizi ya virusi vya
Ukimwi, Hezron alisema takwimu zinazotokana na upimaji wa hiari katika
halmashauri hiyo zinaonesha kuwepo kwa asilimia 9 ya maambukizi.
Katika kipindi cha Januari na Desemba
mwaka jana, jumla ya watu 10,414 walipima kwa hiari na kwa kupitia
kampeni maalumu katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na kati
yao 943 waligunulika kuwa na maambukizi ya VVU.
Hata hivyo alisema utafiti wa kitaifa
unaonesha wilaya hiyo ina asilimia 15.7 ya maambukizi ya VVU kama ilivyo
kwa wilaya nyingine za mkoa wa Iringa na Njombe.
