Baadhi ya Wamiliki wa vyombo vya habari vya televisheni nchini
wamesema watafunga biashara ya kuonesha matangazo iwapo serikali
haitawasha mtambo wa analogia ili kwenda sambamba na uliopo sasa wa
digital.
Hali hiyo imefikiwa baada ya wamiliki hao kuona biashara yao inashuka
na kukimbiwa na wateja wao kutokana na matangazo yao kuwafikia wananchi
wachache tofauti na matarajio ya wadhamini wao kama ilivyokuwa kabla ya
kuzimwa mtambo wa analogia.
Mwenyekiti wa wamiliki wa vyombo vya habari nchini Moat na Mmiliki wa
kampuni ya IPP Reginald Mengi ameishauri serikali iwashe mtambo huo uwe
sambamba na uliopo sasa wa digital ama watoe ruzuku ya ving’amuzi kwa
wananchi ili kila mtu apate haki yake ya kupata habari kama ilivyokuwa
awali.
Nae Mkurugenzi wa kampuni ya Sahara Media Samwel Nyara amesema serikali haikuwa na sababu ya kuharakisha kuzima analogia na kuwapa tabu wananchi wake ambao sasa wanakosa haki ya kupata matangazo kutokana na kushindwa kumudu gharama za ving’amuzi hivyo ameshauri uongezwe angalau mwaka mmoja kwa ajili ya maandalizi.
Tangu kuzimwa kwa mtambo wa analogia Desemba 31 mwaka jana, idadi ya
watazamaji wa televisheni jijini Dar es salaam imeshuka kwa kiasi
kikubwa kutokana na wananchi waliowengi kushindwa kumudu gharama za
kununua ving’amuzi hali inayosababisha wakose haki yao kikatiba ya
kupata habari.
