Na Muhidin Michuzi
MKE wa
Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amewataka akinamama wanaojihusisha na
shughuli za ujasiriamali kuwa waaminifu kwa wenza wao na wanafamilia wao
ili waweze kupata ushirikiano kutoka kwao.
Alisema
mbali ya majukumu mengi yanayowakabili, akinamama wanapaswa kuwa karibu
na familia zao kwani ndiyo msingi mkuu wa Taifa. “Hatuna budi kutoa
malezi mema kwa wenza wetu na watoto wetu. Tunapofanikiwa katika
shughuli zetu, tusiache kuwa waaminifu kwa wana-familia wetu (akinababa
na watoto wetu); tuwaheshimu na kuwaenzi kwa kuwashirikisha kazi
tunazofanya ili tuweze kupata ushirikiano wao na baraka zao,” alisema.
Mama
Pinda ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumamosi, Machi 10, 2013) wakati
akizungumza na wanawake wajasiriamali walioshiriki Maonyesho Maalum ya
Batik (Batik Gala Night) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani kwenye ukumbi wa Hellenic Club, Upanga jijini Dar es
Salaam.
Maonyesho
hayo yaliandaliwa na Kamati ya Tamasha la Wanawake Wajasiriamali
Tanzania (MOWE) kwa kushirikiana na Ofisi ya Shirika la Kazi Duniani
hapa nchini (ILO) yalikuwa na nia ya kuamsha chachu ya kuendeleza kazi
za akinamama wanaofanya maonyesho kila mwaka yaliyopangwa kufanyika
Oktoba, mwaka huu kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema
akinamama wanapaswa kuungana kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze
kuunganisha ujuzi, stadi walizonazo na kushirikishana uzoefu. Alisema
hawana budi kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozalisha zinakuwa na ubora wa
kiwango cha juu ili waweze kukabiliana na ushindani kwenye soko.
“Napenda
kusisitiza, suala la ubora wa bidhaa tunazozizalisha kwa kuzingatia
viwango vya Kitaifa na kimataifa ili bidhaa zetu ziweze kupata uhakika
wa soko. Hili litafanikiwa pia endapo tutazingatia pia ubora wa
vifungashio tunavyotumia kwenye bidhaa zetu. Endapo, tutazingatia
viwango, vifungashio na kutumia kiandishi-anuani (barcodes), sioni ni
kwa nini bidhaa zetu zisiende hadi masoko ya mbali huko ughaibuni,”
alisema.
Aliwataka
akinamama wajipange vizuri kwa ajili ya Maonyesho makubwa ya kitaifa
(MOWE) yatakayofanyika Oktoba mwaka huu ambayo yatajumuisha washiriki
kutoka mikoa yote hapa nchini.
Mapema,
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi hapa nchini (ILO Tanzania), Bw. Alexio
Musindo, alisema anawapongeza akinamama wajasiriamali chini ya kamati ya
MOWE kwani kupitia mafunzo yanayodhaminiwa na Ofisi yake, akianamama
hao wameweza kujiamini zaidi na kuthubutu kushiriki maonyesho mbalimbali
ndani na nje ya nchi.
Alisema
jamii haina budi kuwekeza zaidi kwa wasichana kwa kuwapa fursa za
kujiendesha kibiashara pamoja na ujuzi (skills) ili waweze kujiajiri
kwani wanakumbana na vikwazo vingi wanapotafuta ajira ikiwemo,
unyanyasaji na unyanyapaa.