Na Ibrahim Yassin, Mbarali
WADAU mbali
mbali wakiwemo Madiwani kutoka Wilayani
Mbarali Mkoani Mbeya wamepewa semina elekezi juu ya kuzingatia uchafuzi wa mazingira ili kuepukana na
magonjwa ya kuambukizwa.
Akizungumza jana wakati
wa warsha ya siku moja ya uhamasishaji wa maji na usafi wa mazingira iliyofanyika katika ukumbi
wa Kiluteli iliyopo wilayani humo, muwezeshaji wa warsha hiyo Afisa afya Mkuu mstaafu
Bartholomayo Ngaeje alisema kuwa viongozi hao wanapaswa kuchukuwa hatua
madhubuti katika kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua umuhimu wa usafi
na mazingira.
Ngaeje
alisema kuwa iwapo viongozi watawajengea wananchi hofu ya kuchafua mazingira baadhi ya magonjwa
katika jamii yatapungua kwa kiasi kikubwa kwa kuwa magonjwa mengi yanatokana na
uchafuzi wa mazingira.
Muwezeshaji
huyo
alisema kuwa kuwa hivi sasa kumekuwepo na ongezeko kubwa la watoto
mashuleni lakini ongezeko hilo haliendani na idadi ya vyoo vilivyopo
kwenye shule hizo jambo ambalo linahatarisha afya za watoto.
Alisema kuwa
katika utafiti uliofanywa mwaka 2009 na Shirika la kimataifa UNICEF kwa wilaya
16 nchini zilibaini kuwa asilimia 20 ya wananfunzi hutumia tundu moja la choo kwa wanafunzi 100.
Aliongeza kuwa
katika utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 92 ya shule katika wilaya hizo
hakuna huduma ya kunawa maji na usafi wa mazingira na kuongeza kuwa asilimia
60 ya walimu hawajui suala la usafi wa mazingira.
Alisema kuwa
kuwepo maji ya kunawa kwenye shule unasaidia kupunguza wadudu ambao wanakuwepo
kwenye mikono ambayo ni michafu hivyo kupelekea kupunguza kwa magonjwa kama ya
Kuhala, Kichocho, Kifua Kikuu na mengine ya kuambukizwa.
Aidha alisema
kuwa idara ya elimu inapaswa kutoa muongozo wa kukagua mazingira ya shule
badala ya kuwakagua walimu tu bali hata kufahamu hali ya vyoo na mazingira ya
shule, kwa kusaidiana na ma bwana afya.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbarali Henry Ndingo alisema kuwa elimu
walioipata wanapaswa kuipeleka kwa wananchi ili nao waweze kufahamu umuhimu wa
kutunza mazingira.
Aliongeza kuwa
kila mwanasiasa yeyote anaposimama kwenye majukwa analazimika kuanza kwanza
kutoa elimu ya kutunza mazingira na baada ya hapo ndipo aendelee na siasa zake.
