OCS Francis Massawe
Jamii imetakiwa kuona umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi
wanaorubuniwa na watu kujiingiza katika vitendo vya ngono ilihali wao ni
wanafunzi na kutoa taarifa hizo kwa vyombo vya usalama ikiwemo polisi ili hatua
za kisheria zichukuliwe kwa wahusika
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa kituo cha polisi Matamba
wilayani Makete OCS Francis Massawe wakati akizungumza kwenye kikao cha wadau
wanaotekeleza mradi wa shule salama unaotekelezwa katika kata ya matamba chini
ya shirika la SUMASESU kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa kata hiyo
Bw. Massawe amesema kumeibuka wimbi la watu kujihusisha
kimapenzi na wanafunzi huku wengine wakiwatorosha wanafunzi hao kwenda nao
Mbeya kufanya starehe huku wengine wakitoka na wanafunzi maeneo mengine ya
wilaya ya makete na kuja kukaa nao Matamba na kasha kuwarudisha walikowatoa
“Unakuta wengine wanatoroka na wanafunzi kwenda nao Mbeya na
wengine wanatoka maeneo mengine kama makete mjini halafu wanakuja nao hapa
Matamba kula raha na ilihali ni wanafunzi” alisema Massawe
Amesema kwa mujibu wa sheria mtu chini ya miaka 18 hana
maamuzi na mwili wake hivyo yeyote atakayefanya naye ngono ametenda kosa la
jinai ambalo ni ubakaji bila kujali kuwa mtu huyo alikubali mwenyewe kufanya
mapenzi na mtu huyo
Massawe amesema kwa kiasi kikubwa jamii inawafahamu watu hao
hivyo ushirikiano baina ya wananchi na jeshi la polisi utasaidia kutokomeza
hali hiyo inayodidimiza maendeleo wilayani Makete
Katika hatua nyingine mkuu huyo amekemea tabia ya wananchi
wanaochochea kukwamishwa kwa shughuli za kimaendeleo na kusema ni kosa la jinai
na yeyote atakayehusika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake
Amesema wapo baadhi ya watu kwenye jamii wanapandikiza
habari za uongo kuhusu jambo Fulani la kimaendeleo ili jambo hilo lisifanyike
na kusema kitendo hicho ni cha uchochezi na yeyote atakayebainika kufanya hivyo
atachukuliwa hatua kali za kisheria
Hata hivyo ameitaka jamii kutoa taarifa polisi ikiwemo kuwataja
baadhi ya wahalifu waliopo katika jamii kwani wao ndio wanawafahamu zaidi
kuliko polisi hivyo hatua hiyo itasaidia kupambana na vitendo vya uhalifu