Mkurugenzi wa SUMASESU, Bw. Egnatio Mtawa
Shirika la SUMASESU lililopo wilayani Makete limekanusha
uvumi ulioenea katika kata ya Ikuwo wilayani hapo kuwa shirika hilo ni freemasons
Akizungumza kwenye kikao cha kamati tendaji ya mradi wa
shule salama kilichofanyika katani hapo, Mkurugenzi wa shirika la SUMASESU
Egnatio Mtawa amesema shirika hilo halina uhusiano wowote na freemason na
halitakuja kujihusisha na imani hizo
“Naomba niseme mbele ya kikao hiki SUMASESU hatuna imani za
freemason na hatukijui kitu hicho, mimi nashangaa watu wanaotuhusisha na imani
hizo hawatakii mema maendeleo ya wilaya yetu” alisema Mtawa
Amesema suala hilo limeibuka kufuatia shirika hilo
kutekeleza mradi huo wa shule salama katika shule za sekondari na vijiji
vilivyopo tarafani humo, ambapo pamoja na mambo mengine shirika linagawa
chakula kwa washiriki jambo ambalo linatiliwa shaka na baadhi ya wananchi
“Watu wanakuwa na mawazo ambayo tunashindwa kuyaelewa, eti
shirika linagawa chakula kwa washiriki hasa wanafunzi katika shule
zinazotekeleza mradi, na wakati mwingine zinatolewa posho kwa wawesheshaji
ngazi ya vijiji, eti kwa kuwa shirika linafanya hivyo sisi ni freemason kitu
ambacho si kweli” alisema
Amesema suala hilo ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha
shughuli za kimaendeleo wilayani makete hivyo wananchi wanapaswa kuondokana na
imani hizo na badala yake kuunga mkono jitihada za shirika na serikali kwa
ujumla kutoa elimu ya unyanyasaji wa kijinsina na VVU/UKIMWI
Kwa upande wake afisa mtendaji kata ya Ikuwo Bw. Guerino
Mwasanga aewataka wananchi kupuuza suala hilo kwa kuwa halina uhusiano wowote
na shughuli za maendeleo katani kwake, na kuwataka wananchi wote kuungana kwa
pamoja ili lengo la mradi huo liweze kutimia