Polisi mkoani Pwani imesema
imekamilisha uchunguzi dhidi ya vijana watatu wanaotuhumiwa kumteka na
kumbaka binti wa miaka 16 huku wakimfungia ndani bila ridhaa yake kwa
miezi minne.
Pamoja na hayo, wanaharakati na wanasheria wametoa maoni yao kuhusu tukio hilo, ambapo pamoja na kulaani wahusika, pia wametaka taratibu za kisheria zifanyike haraka ili watuhumiwa wakibainika kuhusika wachukuliwe hatua kali.
Akizungumza na mwandishi jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema kwa mujibu wa utaratibu wa sasa, polisi wanapokuwa na kesi lazima waiwasilishe kwanza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ndipo ipangiwe tarehe ya kufikishwa mahakamani.
“Sisi tuko tayari, tumeshapeleka jalada kwa wanasheria, tunachosubiri ni tarehe ambayo watuhumiwa hawa watapandishwa kizimbani,” alisema Matei.
Alisema uchunguzi wa awali wa Polisi umebaini kuwa watuhumiwa hao; Faida Kazigwa, Isaka Kazigwa na Jovian Oswald wanatakiwa kujibu mashitaka ya kuteka na kubaka.
Mwanasheria wa kujitegemea, Rosalie Makalle alilielezea tukio hilo kama la kuteka na kubaka, ingawa aliahidi kufuatilia kwanza mkasa huo ili kutathmini sheria inasemaje.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Valeria Msoka, alisema kitendo alichofanyiwa binti huyo ni unyama na kutaka vyombo vya sheria kuharakisha kesi hiyo na hukumu itolewe mapema.
“Unajua vitendo hivi vinakithiri sana siku hizi kwa kuwa kesi za aina hii zinapofika kwenye vyombo vya sheria huchukua muda mrefu hadi kupatiwa ufumbuzi, hivyo ni vema katika hili muda ukazingatiwa na iwapo wahusika watabainika kuwa na makosa wapewe adhabu kali ili iwe fundisho,” alisisitiza.
Vijana hao wanadaiwa kuwa Novemba 11 mwaka jana walimteka na kumweka kwenye mazingira magumu mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa sekondari Pangani mkoani Pwani na kumbaka na kisha kumtoa mimba kwa kumkorogea majani ya chai na kumnywesha.
Hata hivyo, alifanikiwa kuepuka mateso hayo, pale vijana hao siku moja waliposahau kufunga mlango na yeye kupata upenyo na kutoroka na kuingia porini akiepuka kukutana na vijana hao lakini njiani akasaidiwa na mchoma mkaa kuwasiliana na babu yake na kurejea nyumbani.
Kabla ya hapo, binti huyo alikuwa akichungwa na mmoja wa vijana hao aliyekuwa na kisu, hivyo kumtia hofu na kushindwa kupiga kelele hata watu wakiwamo polisi, walipofika katika kibanda alimokuwa amefichwa kwa muda wote huo.
Babu wa binti huyo, Daudi Zakayo, alisema mjukuu wake alipotea Novemba 3 na walifanya juhudi zote za kumtafuta ikiwa ni pamoja na kuripoti Polisi lakini bila mafanikio.
“Binti huyu ninaishi naye lakini baba yake yuko Ruvu anafanya kazi huko, mama yake hayupo, nilipoona haonekani nilimtaarifu baba yake, Charles Daniel, ambaye alikuja na wote tukaanza kuzunguka mtaani kwa rafiki zake hadi Polisi bila mafanikio,” alisema.
Alisema kutokana na binti huyo kutoonekana kwa muda mrefu, baba yake alikwenda kwa waganga wa jadi na mmojawao kudai yuko maeneo hayo amefichwa kwenye mti, lakini hata mganga huyo alipofanya ‘mambo yake’ bado hakuonekana.
SOURCE:HABARILEO