Na Anna Nkinda – Sumbawanga
Watoto wa kike nchini wametakiwa
kuepukana na vishawishi vya chips Kuku, lifti, simu za mkononi na zawadi
za aina mbalimbali wanazorubuniwa nazo kwani vitu hivyo havina nia
njema ya kumkomboa msichana kielimu, kijamii na kiuchumi zaidi ya
kumuharibia mpango mzima wa maisha yake.
Onyo hilo limetolewa jana na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanafunzi wa kike zaidi ya
1000 kutoka shule mbalimbali za mkoa wa Rukwa katika viwanja vya shule
ya Sekondari ya wasichana ya mtakatifu Theresia iliyopo mjini
Sumbawanga.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kwamba watoto wengi
wa kike wanashindwa kumaliza masomo na kufikia malengo kutokana na
changamoto zinazowakabili ambazo nyingi siyo za kitaaluma japo
zinaathari nyingi kitaaluma, kiafya na kimaendeleo.
“Tunafahamu kuwa wanafunzi wengi
hupata vishawishi ambavyo huwapelekea kupoteza umakini, muelekeo na kuwa
watoro, kupata ujauzito, maambukizi ya Ukimwi na hatimaye kupoteza
fursa hii adimu na adhimu ya elimu ya Sekondari na dira ya maisha yao.
Ni muhimu kujidhatiti na kujiepusha na mitego, vishawishi na matendo
yanayoweza kusababisha matatizo haya.
Msikubali vishawishi kwani peremende
ya dakika si sawa na asali ya maisha.Iweje uridhie kuuharibu mpango wa
maisha yakokwa kitu cha mara moja? Licha tu ya kuwa atakayehusika na
kosa la kukupa mimba anapaswa kushtakiwa kisheria, lakini kwako wewe ni
hatari kiafya kwani kushika mimba ukiwa na umri mdogo unahatarisha
maisha yako wakati wa kujifungua. Asilimia ishirini ya vifo vya akina
mama wajawazito hutokana na uzazi katika umri mdogo”, alisema Mama
Kikwete.
Aidha Mama Kikwepi pia aliwataka
wanafunzi hao kuwatii wazazi wao,kusoma kwa bidii na kujiamini kwamba
wanaweza kwani chochote anachoweza kufanya mtoto wa kiume kitaaluma na
halikadhalika mtoto wa kike anaweza kukifanya hivyo basi wasome zaidi
masomo ya sayansi na hisabati kama watoto wa kiume.