Diwani wa kata ya Unyamikumbi Mosses
Shaban Ikaku, akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa
manispaa ya Singid. Kikao hicho kilikuwa maalum kwa ajili ya kupitisha
bajeti ya manispaa ya Singida kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.(Picha na
Gasper Andrew).
Na Nathaniel Limu.
Watendaji wa halmashauri ya manispaa
ya Singida wameshauriwa kujenga utamaduni wa kusimamia kikamilifu
misaada mbalimbali inayotolewa na mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh.
Mohammed Dewji, ikiwemo ya sekta ya kilimo ili manispaa hiyo iweze kupaa
kimaendeleo.
Rai hiyo imetolewa na diwani (CCM)
kata ya Unyamikumbi Moses Shaban Ikaku, wakati akizungumza kwenye kikao
maalum cha madiwani ambacho kilipitisha bajeti ya manispaa ya Singida
kwa kipindi cha 2013/2014.
Amesema misaada mingi na mikubwa
inayotolewa na mbunge Dewji yenye lengo la kuwapatia wananchi maendeleo
endelevu, haijafikia malengo yanayokusudiwa.
Moses amesema kwa utafiti na uzoefu
wake, miradi hiyo imekuwa haitoi matunda mazuri kutokana na sababu kuu
moja, nayo ni watendaji/wataalam kutoisimamia kikamilifu.
Diwani huyo meisema mfano hai na
mzuri, ni wa msaada wa hivi karibuni wa majembe ya kukokotwa na ng’ombe
zaidi ya 500 na zaidi ya tani 60 za mbegu bora za dengu, choroko na
mbaazi.
Moses amesema msaada huo wenye thamani
kubwa na ambao ulikuwa na sharti nafuu ambalo ni wakulima 10 kujiunga
kwenye kikundi, kama ungesimamiwa kikamilifu na wataalam wa kilimo na
watendaji wengine, ungewakomboa kiuchumi wakazi wa jimbo la Singida
mjini.
Aidha, amesema endapo majembe hayo
yangetumika ipasavyo, ingechangia wakulima kulima kisasa na kupanua
ukubwa wa mashamba yao, kitendo ambacho kigesaidia wakulima kupata
mapato makubwa na kupelekea kununua trekta kubwa.
“Nachukua fursa hii kumshukuru na
kumpongeza mbuge wangu Mh. Dewji , kwa kugawa majembe zaidi ya 500 ya
kukokotwa na wanyama kazi, lengo lake ni zuri mno, kwa sababu analenga
kusaidiana na serikali katika kufikia malengo ya kilimo kwanza. Lakini
nasikitika sana, kusema msaada huu huenda usizae matunda mazuri kwa
sababu hausimamiwi kikamilifu na wataalam wa kilimo na watendaji
wengine”amesema Moses kwa masikitiko.
Amesema msaada huo na mingine mingi
inayotolewa na Mh. Dewji, imekuwa kama ni kiini macho mbele ya wataalam
na watendaji wa manispaa, na kwa sababu hiyo, imekuwa haifikii lengo.
Moses amesema wakilitambua hilo na
wakasimamia misaada inayotolewa kwa wananchi ipasavyo, misaada hiyo
itakuwa na tija zaidi kwa maana kwamba itasaidia kupaisha maendeleo ya
wananchi.
Pia kwa njia hiyo, itamvutia zaidi
mbunge Dewji na wadau wengine kuongeza misaada zaidi ambayo itawakwamua
wananchi kutoka kwenye lindi la umaskini.