Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Wanzanzibari kuitumia
fursa ya kupata vitambulisho vya Taifa kwani ni haki yao kikatiba na
kuachana na propaganda za baadhi ya watu kulihusisha zoezi hilo la
Vitambulisho vya Taifa na itikadi za kisiasa. Dk. Shein aliyasema hayo
leo huko katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi, viliopo Chukwani
Mjini wa Zanzibar. Katika Sherehe za utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alirejea kauli yake ya kuwahakikishia
wananchi wa Zanzibar kuwa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi vitaendelea
kuwepo na kutumika kwa madhumuni yaliokusudiwa kwa mujibu wa Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984.
Alisema kuwa uzoefu wa makosa yaliyotokea wakati wa usajili wa
Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi utumike ili kuondoa kasoro na matokeo
yatakayoathiri kupatikana ufanisi katika kuendesha zoezi hilo la
Vitambulisho vya Taifa.
Alieleza kuwa kuwepo kwa vitambulisho vya Taifa, kutaisaidia Serikali
katika kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yake na hivyo kuweza
kuziimarisha huduma za kijamii, kama vile elimu, afya na upatikanaji wa
maji safi na salama.
Aidha, alisisitiza kuwa mapato hayo yatasaidia kuimarisha miundombinu
ya barabaram huduma za umeme na pia, kuimarisha ulinzi wa raia na mali
zao kadhalika itakuwa ni rahisi katika kukabiliana na tatizo la
wafanyakazi hewa jambo ambalo hupelekea serikali kupoteza fedha nyingi.
Dk. Shein aliwakumbusha watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA) kuendeleza umakini na uadilifu walio nao, kwa kutambua
dhamana kubwa waliyonayo kwa niaba ya Watanzania.
“Kazi yenu inahitaji uzalendo, ustahamilivu na kuweka mbele maslahi
ya nchi badala ya maslahi binafsi, jambo ambalo sina shaka mnalielewa
vyema na mtalitekeleza, lakini ni wajibu kukumbushana kwani, tunaambiwa
kuwa ukumbusho huwafaa walioamini”alisema Dk. Shein.
Aidha, kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa wananchi wake
hawana budi kuzingatia kuwa kutokana na nchi yenyewe ni ya visiwa
haiwezi kuhimili ongezeko lkubwa la watu kutokana na rasilimali zilizopo
hasa rasilimali ya ardhi.
