WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameendesha harambee ya papo hapo na
kufanikiwa kuchangisha sh. milioni nane kwa ajili ya ukarabati wa pampu
za visima tisa vya maji kwa wakazi wa kijiji cha Magamba, kata ya
Magamba wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Waziri Mkuu alilazimika kuendesha harambee hiyo jana mchana
(Jumapili, Januari 6, 2013) wakati akijibu hoja za wakazi wa kata hiyo
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya
sekondari Magamba wilayani Mlele.
Kaimu Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo, Bw. Enock Msengi alisema
wanakijiji hao kupitia kamati ya maji walikuwa na sh. 150, 000/- kwenye
akaunti yao. “Kama wangekuwa na fedha walau sh. milioni tatu, tungemudu
baadhi ya gharama, lakini kwa hizi fedha alizochangisha Waziri Mkuu,
tunaweza kukarabati visima vyote na vikafanya kazi… vinavyohitajika
zaidi ni vipuri vya pampu,” alisema mara baada ya mkutano huo.
Akizungumza na wakazi hao, Waziri Mkuu aliwasisitiza watumie kilimo
cha sesa ili kiwe mkombozi wao. Alipowaita mbele ya hadhara mabalozi wa
mashina 18 na kuhoji kila mmoja wao analima ekari ngapi na anatumia
kilimo gani, alibaini kuwa ni balozi mmoja tu ambaye anatumia kilimo cha
sesa na amepanda kwa mistari na kutumia mbolea.
“Hawa wana ekari moja hadi ekari tano lakini wengi wao mmesikia ni
matuta, matuta, matuta hata kwenye karanga wametumia matuta. Nawasihi
sana mwakani kila mmoja atumie kilimo cha sesa kwa sababu kina tija
zaidi kuliko hayo matuta… yanapoteza sehemu kubwa ya ardhi ya kilimo,”
alisisitiza.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa anamalizia ziara yake ya jimbo kwenye kata
mbili kati ya 14 zilizobakia wakati wa ziara yake Desemba mwaka jana,
aliwasihi mabalozi hao watumie umoja wa kikundi chao cha kilimo
kuelimishana na akaahidi kuwatafutia majembe ya kukokotwa na ng’ombe
ikiwa ni pamoja na kuwanunulia maksai ili waboreshe kilimo na wawe
viongozi wa mfano.
Alipouliza kuna wafuga nyuki wangapi kwenye mkutano huo, walijitokeza
wanane ambao jumla yao walikuwa na mizinga ya asili 34. Yeye aliahidi
kuwapatia mizinga 50 ya kisasa (ya vibao na ya ngazi) ili waboreshe
ufugaji wao.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kuhimiza ujasiriamali kwa
kuwaunga mkono akinamama wa Magamba ambao wanauza matunda na kuahidi
kuwapatia sh. milioni tano ili ziwasaidie kuboresha biashara zao lakini
akawataka waunde umoja, wachague viongozi na kuchangishana fedha za
kianzio.
“Hapa Magamba siyo mbali na Mpanda mjini ambako yako Makao Makuu ya
Mkoa… ninyi mnaweza kuwa chanzo kizuri cha kuwalisha wale watu wa mjini
matunda na mbogamboga kwa sababu ya mabonde mliyonayo, tumieni hiyo
fursa vizuri,” aliwasisitizia.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua shamba la miembe ya kisasa la shule ya
sekondari Magamba na kuahidi kuwaongezea miche mingine 100. Wakati
linaanzishwa Desemba 15, 2010, shamba hilo lilikuwa na miche 80 lakini
11 imekufa na imebakia 69. Wanatarajia kuanza kuvuna maembe ya kwanza
Desemba, mwaka huu.
Short URL: http://www.thehabari.com/?p=27113