NUSU ya watu wanaotumia kondomu kwa ajili ya
kujikinga na mimba ama magonjwa ya zinaa, hawajui namna ya kuitumia
mipira hiyo, utafiti umeeleza. Utafiti huo mpya ulifanywa na Dk
Stephanie Sanders wa Taasisi ya Kinsley inayohusika na Utafiti wa
Masuala ya Jinsia, Jinsi na Uzalishaji katika Chuo Kikuu cha Indiana.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa katika nchi 14 ikiwamo Tanzania
katika kipindi cha miaka 16 iliyopita kuanzia mwaka 1995 hadi 2011, watu
wengi wamekuwa wakifanya makosa kwa namna mbalimbali katika kutumia
kandomu ikiwamo uvaaji.
“Makosa yanayofanywa mara kwa mara na watumiaji wa kondomu ni pamoja
na kuingiza kinga hiyo nusu katika uume wakati wa ngono au kuitoa kabla
tendo hilo halijamalizika au kusubiri mpaka isinyae,” imesema sehemu ya
utafiti huo. Makosa mengine ni kutoacha nafasi katika ncha ya kondomu
kwa ajili ya mbegu za kiume na kuzifungua vibaya katika pakiti yake.
Jambo hilo linalosababisha kucha kuzitoboa na hatimaye kupitisha
mbegu au majimaji kwenda kwa mwanamke,” umeeleza utafiti huo. Utafiti
huo umeonyesha kuwa makosa mengine ni kuigeuza kondomu ndani-nje,
kuihifadhi katika sehemu isiyostahili na kurudia kuitumia katika tendo
lingine la ngono.
Kuivua vibaya: Asilimia 57 ya watu waliohojiwa, walikiri kuvua
kondomu kimakosa baada ya tendo la ngono. Kati yao asilimia 27 walikuwa
wanawake na asilimia 31 ni wanaume. Pamoja na makosa hayo ya uvaaji wa
kondomu, watafiti nchini India wanatarajiwa kufanya utafiti mwingine
mkubwa kuhusu suala hilo kubaini sababu yake.
Watafiti hao waliamua kufanya uchunguzi baada ya kubainika kuwapo kwa
wanaume ambao maumbile yao ni makubwa au madogo kuliko mipira hiyo ya
kiume. Hata hivyo, kondomu zinazopatikana nchini Tanzania hazitofautiani
ukubwa.
Dk Sanders alisema makosa yanayofanywa wakati wa kutumia mipira hiyo
yanachochewa na watumiaji wenyewe na kukosekana kwa msisitizo wa elimu
ya namna ya kuzitumia kondomu hizo kutoka kwa watengenezaji au taasisi
za Ukimwi.
Makundi tofauti yalijumuishwa katika utafiti huo wakiwemo wanandoa,
wafanyabiashara ya ngono na wanafunzi wa vyuo. Kati ya asilimia 17 na
51.1 ya watu walioulizwa maswali katika utafiti huo walikiri kuwa
huingiza kondomu nusu katika uume wakati wa tendo la ngono.
CHANZO: Gazeti Mwananchi