WAHADZABE MKOANI MANYARA WAJIPANGA KUACHANA NA MAISHA YA UWINDAJI

 
JAMII ya wahadzabe iliyopo eneo la Bonde la Yaeda Chini Wilayani Mbulu,Mkoani Manyara imejipanga kikamilifu kuachana na maisha ya uwindaji,kurina asali,kuokota matunda na kugeukia kilimo cha chakula.
 
Aidha kutokana na hivi sasa kutoweka kwa wanyamapori hasa nyani pamoja na tembo waliomalizwa na wawindaji haramu (majangili) na kutopatikana kwa urahisi kwa matunda ya mibuyu kumewasababisha wageukie kwenye kilimo.
 
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbulu Anatory Choya wakati akiongea mbele ya jamii hiyo ya wahadzabe alisema kuwa wamewapatia majembe 200 kwaajili ya kulima kwa mikono pamoja na kilo 500 za mbegu ya mtama kwa ajili ya kilimo.
 
Mkuu wa wilaya hiyo aliendelea kusema kuwa wametekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa mwishoni mwa mwaka jana la kubadilisha maisha ya jamii ya wahadzabe kutoka kutegemea kuokota matunda,kurina asali na uwindaji hadi kulima.
 
“Jamani kupitia kilimo jamii ya wahadzabe hivi sasa itabadilika kwa kulima chakula chao kuliko ilivyokuwa hapo awali na pia baada ya kugawa vifaa hivyo kwenye kata hii ya Yaeda Chini na kugeukia kata ya Eshkesh” alisema Choya.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji cha Mongoamono kata ya Yaeda chini Gidabodigi Gidahonda ameishukuru Serikali kwa kutoa msaada huo kwa jamii hiyo na kuahidi kuutumia vizuri kwa lengo lilivyokusudiwa.
 
Aidha aliongeza kuwa baada ya serikali kugawa majembe hayo 200 ambapo kila kaya itapata majembe mawili yaani baba jembe moja na mama jembe moja watayatumia kwa kulima kwani wanayo ardhi kubwa ya kutosha kwa kilimo.
 
Naye mmoja kati ya wakazi wa kijiji cha Mongoamono ambaye ni jamii ya wahadzabe Therathini Nkwemo mwenye umri wa miaka 90 amemshukuru mkuu wa wilaya hiyo Choya kwa kuwapatia majembe kwani awali aliwapatia chakula kilichowasaidia wakati wa njaa.
 
“Tunamshukuru mkuu wa wilaya kwa msaada wake kwetu kwani hivi sasa badala ya sisi kumiliki mishale na pinde tutakuwa tunamiliki majembe ambayo yatatusaidia kulima mashamba na kupata chakula,” alisisitiza Nkwemo.
 
Nao baadhi ya wakazi wa mkoa wa Manyara wanasubiri kwa hamu utekelezaji wa hatua hiyo ya kujiunga na ukulima kwani mwanzoni mwa mwaka 2,000 baadhi ya jamii ya wahadzabe walijengewa nyumba za bati na wakagoma kuzitumia.
 
Jamii ya wahadzabe ni miongoni mwa jamii zilizo na idadi ya watu wachache nchini,kwani kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 jamii hiyo ilikuwa na watu wasiozidi 1,000 na hawana utamaduni wa familia kuzaliana kwa wingi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo