Dar es
Salaam
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Philipo Mulugo ametangaza
matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Sekondari Kidato cha Pili mwaka
2012, ambapo kiwango cha ufaulu kimepanda kutoka asilimia 45.40 mwaka
2011 hadi kufikia asilimia 64.55 mwaka 2012.
Matokeo hayo yametangazwa mbele ya waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam ambapo idadi ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani
walikuwa 430,327, kati yao wasichana walikuwa 205,476 na wavulana
224,851, ikiwa ni upungufu wa watahiniwa 36,240 ikilinganishwa na
mwaka 2011 ambao walikuwa 466,567.
“Watahiniwa 386,271 sawa na asilimia 89.76 ya waliosajiliwa, walifanya
mtihani wakiwemo wasichana 187,244 na wavulana 199,027, watahiniwa
44,056 sawa na asilimia 10.24 hawakufanya mtihani, kati yao wasichana
ni 18,231 na wavulana 25,825” amesema Mulugo.