Serikali imeombwa
kuharakisha uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata ya Bashnet iliopo wilaya
ya
Babati mkoani Manyara ili waweze kumpata diwani atakayesimamia
maendeleo
katika kata yao.
Wakiongea
na waandishi wa habari wakazi wa kata hiyo walisema
kuwa hivi sasa hawana diwani baada ya hivi karibuni aliyekuwa diwani
wao
Laurent Tara kuhama chama cha NCCR-Mageuzi na kuhamia Chadema hivyo
kupoteza
udiwani wake.
Aidha
walibainisha
kuwa kwa vile Tara
alikuwa diwani wao kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi tangu mwaka 2000 hadi
Desemba 17
mwaka jana,wanatarajia kumchagua tena kupitia Chadema kwani amewaletea
maendeleo makubwa ikiwemo suala zima la elimu.
Naye
mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya
Babati Vijijini Nicodemus Tarmo amethibitisha kupokea barua ya Tara
kujiuzulu
nafasi ya udiwani baada ya kuhama NCCR-Mageuzi hivyo kupoteza sifa ya
kuwa
diwani.
Alisema
kuwa wameshaandika
barua kwenye ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwajulisha kwamba kata ya Bashnet
hivi
sasa haina diwani baada ya Tara kujitoa kwenye chama kilichompa ridhaa
ya
kuongoza wananchi.
Alibainisha
kuwa suala la kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya kumpata
diwani wa kata hiyo linasubiri utaratibu kutoka Tume ya Taifa ya
uchaguzi baada
ya kupata barua kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.
Naye mmoja kati ya wakazi hao Abraham Mlundi
alieleza
kuwa tangu Tara awe diwani wao amefanikiwa kusimamia ujenzi wa shule
tano
za sekondari na shule 13 za msingi hivyo kufanya kata hiyo kuwa na
sekondari
nyingi zaidi katika mkoa huo.
Alisema kuwa Tara ni diwani ambaye amejitahidi
kuleta
maendeleo kwenye kata hiyo hivyo wanaiomba Serikali iharakishe uchaguzi
ili
wapate mwakilishi kwani hivi sasa wamebakiwa na diwani wa viti maalum
Angela
Pius.
Kwa upande
wake Mchungaji Wemaeli Sarwat wa kanisa la Pentekoste Bashnet alieleza
kuwa
kata hiyo itakuwa na pengo lisiloweza kuzibika baada ya Tara kujiuzulu
kwani alikuwa anajulikana kwa jina la bwana maendeleo.
Noberk
Lucas ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Guse (CCM) alisema kuwa
Tara ameacha mambo mengi ya maendeleo ya kukumbukwa ikiwemo kilimo bora
na kupigania haki za binadamu kwa kutoa elimu ya uraia.
“Pia
alishiriki kufanya mageuzi ya kilimo kwa kuwapa mbegu ya viazi mviringo
kutoka
Rongai mkoani Kilimanjaro na badala ya kupata magunia sita wakawa
wanavuna
magunia 25 hadi 30 kwa ekari moja,” alisisitiza Lucas.
