*RC amtetea DC kuhamia Mdandu
Na Waandishi wetu
Wananchi wa Kata ya Igwachanya wanamlilia aliyekuwa Mtendaji wa
Kata yao kwa maelezo kuwa alikuwa mchapakazi.
Taarifa ambazo Kwanza Jamii-Njombe imezipata zinasema Job
Fute amehamishwa kutoka katika kata hiyo kimyakimya baada ya
kulitaarifu gazeti hili juu ya tetesi zilizopo katika kata hiyo juu ya
uamuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe kutokubali nyumba ya mbunge na
kuamua kuanzia shughuli zake kata ya Mdandu.
Imefahamika baada ya Fute kuondolewa katika wadhifa wake kama
mtendaji wa Kata ya Igwachanya, hivi sasa yupo mapokezi katika idara ya
utumishi katika ofisi za Halmashauri kama adhabu.
Hata hivyo, katika mkutano na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Njombe
Kepteni (Mstaafu), Assery Msangi aliwaeleza wananchi wa Igwachanya kuwa,
kitendo cha kuamua kutumia ofisi za Mdandu ni kuepuka matumizi mabaya
ya fedha kwani ingeigharibu wilaya hiyo ya Wanging’ombe kiasi
kisichopungua sh. 90 milioni kuikarabati shule waliyokuwa wamepewa na
kanisa huko Igwachanya.
Msangi aliyetumia
muda mwingi kuelezea kwa nini ofisi ya DC alisema “Maneno yamekuwa
mengi, sasa ni wakati wa kufanya kazi…tumeshatengewa sh.2.5 bilioni kwa
ajili ya kujenga ofisi.”
Hata hivyo aliwataka wakazi hao kukubali madhara yanayotokana na
eneo lao kuwa makao makuu kama kubomolewa nyumba kutokana na upanuzi wa
barabara na pamoja kuanza kulipia huduma kama maji.
Akizungumzia uhamisho wa ghafla wa mtendaji wa kata ya
Igwachanya kwa kueleza ‘ukweli’, Shukuru Martin, mkazi wa eneo hilo
amesema, muda mfupi wa Fute umekuwa na maendeleo ya haraka hasa
uhamasishaji wa uchangiaji wa sekondari.
Alikwenda mbele na kuongeza, wakazi wa eneo hilo hawaoni jambo
baya aliloeleza kwenye gazeti na kuongeza; “tunashangaa serikali
ilivyokuja juu na kumwamisha kiongozi wetu tena bila hata kutuambia
lolote. Sasa tutaona itakavyokuwa sababu hatutamkubali mtendaji yoyote
atakayeletwa kwenye kata hii.”
Naye Athuman Kilamlya, mkazi wa Igwachanya amesema, uamuzi huo
unaonesha pasipo shaka kwamba, serikali haiwapendi viongozi wanaopenda
kusema kama taarifa za Fute alizotoa kupitia Kwanza Jamii-Njombe.
Hildegat Mwanyika alilaumu kitendo cha mkurugenzi kumhamisha
ghafla mtendaji huyo bila kuangalia upande wa pili ambao ni wa wananchi
kwani wanamjua utendaji wake na kumwondoa ni sawa na kuwarudisha
wananchi nyuma kimaendeleo.
“Mkuu wa wilaya alibisha hodi hapa na tulimpokea kwa moyo mmoja
sasa kwanini aondoke tena bila taarifa yoyote? Mtendaji aliongea kwa
niaba yetu sasa kwanini mkurugenzi amwamishe bila hata kusikia lolote
kutoka kwetu, kwa maana hiyo mkurugenzi pia hana nia njema na sisi na
anakubaliana na yale ambayo yataendelea kuturudisha nyuma,” alisisitiza.
Igwachanya ni eneo lililopo Wanging’ombe na Rais Jakaya Kikwete
alitangaza kuwa litakuwa makao makuu ya wilaya. Kutokana na maandalizi
duni ya kulifanya eneo hilo kuwa makao makuu, Mkuu wa wilaya hiyo,
Esterina Kilasi aliamua kuweka ofisi eneo ya Mdandu kwa muda, jambo
lililowatisha wakazi wa Igwachanya kuwa huenda alitaka kuhamia huko moja
kwa moja.
Chanzo: Jamii Kwanza Njombe
