Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (katikati) akiendesha kikao
cha RCC
Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa
wa Iringa wametakiwa kusimamia vizuri miradi na fedha za Serikali ili
kudhibiti
matumizi mabaya na hoja zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokusimamia
vizuri
fedha na miradi hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma, wakati
akifungua
kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo
katika
Wilaya ya Iringa.
Dkt. Christine amesema kuwa katika
agenda zitakazojadiliwa ni utekelezaji wa Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu
wa Hesabu za Serikali.
“Ninalowasihi ndugu wajumbe, kwa mwaka huu,
kuanzia sasa
ni kusimamia miradi na fedha ambazo Halmashauri hupewa na Serikali, ili
kudhibiti ubadhilifu wa fedha na hoja zinazoweza kujitokeza” asilisitiza
Dkt.
Christine.
Aidha, aliwashauri kutokuanzisha miradi mipya wakati miradi
ya
zamani haijakamilika na kuwataka kumaliza miradi viporo kwanza ndipo
waanzishe
miradi mipya.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, aliwashauri wajumbe wa kikao hicho kuwashauri wakulima
wanaoishi katika maeneo yenye upungufu wa mvua, kulima mazao
yanayovumilia
ukame.
Amesema “nichukue fursa hii kuwaomba kufikisha ujumbe kwa
wakulima
wanaoishi maeneo yenye upungufu wa mvua, kuwa ni vizuri wakulima walime
mazao
ya mtama na alizeti ambayo yanavumilia ukame”.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa alitumia kikao
hicho kuwataka wajumbe kusimamia suala la utunzaji wa mazingira ambayo
kwa sasa
yanaharibiwa kwa kasi kubwa na shughuli za binadamu.
Wakati huo huo, Sekretarieti ya Mkoa
wa Iringa imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi 950,000,000 kwa mwaka
wa
fedha 2011/ 2012.
Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji
wa Mpango na bajeti kwa kipindi cha Julai-Juni, 2011/ 2012, Katibu
Tawala
Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Nuhu Mwasumilwe amesema kuwa kwa
mwaka
wa fedha 2011/2012, Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa ilikadiriwa kukusanya
jumla
ya shilingi 903,000.
Amesema hadi kufikia mwezi Juni, 2012 jumla ya
shilingi
950,895,762 zimekusanywa kwa mchanganuo ufuatao, marejesho ya mishahara
ni shilingi
949,591,700, kodi ya pango la nyumba ni shilingi 636,238 na ada ya
ufuatiliaji
shilingi 19,000.