Nape NNauye (CCM)
Mbunge wa Ubungo
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), John Mnyika (picha na Habari Mseto Blog)
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Nape Nnauye Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM kufuatia madai ya uzushi na uongo aliyoyatoa
tarehe 12 Agosti 2012 kuwa anao ushahidi kwamba CHADEMA kimekuwa
kikiwahadaa wananchi kwa kuwachangisha fedha huku kikipokea mabilioni ya
fedha kutoka kwa wafadhili kutoka nje.
Izingatiwe kuwa matamshi yake yalitangazwa na
vyombo vya habari vya kielekroniki ikiwemo vituo vya televisheni, radio
na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii tarehe 12 Agosti 2012 na katika
kurasa za mbele za magazeti mbalimbali tarehe 13 Agosti 2012.
Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA iliagiza
wanasheria wamwandikie barua ya kumtaka kukiomba radhi Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo kwa kutumia njia ile ile aliyotumia kufanya
propaganda chafu za kuikashifu na kuifitisha CHADEMA kwa umma wa
watanzania ikiwemo kuzusha kuwa upo uwezekano wa CHADEMA kupewa fedha
hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani.
Tayari ameshaandikiwa barua ya kisheria tarehe
24 Agosti 2012 ya kumtaka aombe radhi na kulipa fidia ya bilioni tatu
kwa matamshi hayo ya uzushi na uongo yenye maana ya kuwapotosha
waliyoyasikia na kuyasoma kuwa CHADEMA kinawalaghai wananchi, kina
viongozi wasio waaminifu na kwamba kiko tayari kuuza nchi wa uroho wa
madaraka.
Kipaumbele cha
CHADEMA katika suala hili ni kuombwa radhi hata hivyo kiwango cha fidia
ya fedha kwa fedheha kilichotakiwa ni fundisho kuwa uzushi na uongo
unagharimu.
Ikumbukwe kwamba
tarehe 12 Agosti 2012 nilitoa kauli ya awali baada ya mkutano Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo
mengine nilieleza kwamba tutatoa tamko la kueleza hatua za ziada baada
ya kupata taarifa kamili aliyoitoa.
Katika kauli hiyo nilitoa mwito kwa Mwenyekiti wa
CCM Rais Jakaya Kikwete kueleza watanzania iwapo propaganda hizo chafu
zina baraka zake; hivyo ukimya wake mpaka sasa kuhusu matamshi hayo
inakifanya CHADEMA kuwa na imani yenye shaka (benefit of doubt) kwamba
Nape hakutumwa na chama chake kutoa matamshi aliyoyatoa.
CHADEMA inachukua fursa hii kuutaarifu umma
kwamba asipotekeleza matakwa hayo ndani ya siku saba kuanzia tarehe hiyo
aliyopokea barua hatua nyingine ya kumfikisha mahakama kuu zitaanzishwa
ili aweze kuchukuliwa hatua zaidi.
Pamoja na kuchukua hatua za kisheria, CHADEMA
kinaendelea kutimiza dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi,
mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya
Tanzania kwa pamoja na mikakati mingine kutekeleza operesheni ya
vuguvugu la mabadiliko nchini (M4C) na tunawashukuru wananchi kwa
kuendelea kuunganisha nguvu ya umma kwa hali na mali katika maeneo
mbalimbali nchini.
Imetolewa tarehe 26 Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi