RAIS JAKAYA KIKWETE AZINDUA AWAMU YA TATU YA TASAF


RAIS Jakaya Kikwete hii leo amezindua awamu ya tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), ambayo inalenga kutoa fedha moja kwa moja kwa kaya maskini nchini ili ziweze kujikwamua kiuchumi.

Awali mfuko huo ulikuwa ukitoa fedha kwa miradi mbalimbali ya jamii kama ujenzi wa shule, vituo vya afya, nyumba za walimu, ujenzi wa madaraja na miradi ya watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu na watu wanaoishi na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga alisema jijini Dar es Salaam kuwa uzinduzi huo umefanyika mjini Dodoma.

“Awamu ya pili imekuwa na mafanikio makubwa… Madhumuni ya awamu ya tatu ni kuendeleza mafanikio yaliyopatikana awamu ya pili ili kuwezesha kaya maskini  kuongeza kipato na fursa za kuinua kiwango cha matumizi yao.” alisema Mwamanga.

Alisema awamu hii itaendeshwa kwa kipindi cha miaka 10 na itakuwa na awamu mbili za miaka mitano mitano.

Ili kufanikisha mpango huo, alisema hadi jana, wafandhili pamoja na Serikali, walikuwa wamechangia Dola za Marekani 272.9 milioni karibu na Sh 436.64 bilioni.

Alisema fedha hizo zitatumika kwenye kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya awamu hiyo.

Mtindo wa Tasaf kuzisaidia familia masikini moja kwa moja, alisema ulitokana na mradi wa majaribio uliofanyika wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili na kuonyesha utaweza kuondoa umasikini unaozikumba kaya nyingi nchini.

Mkakati huo aliuelezea utasaidia kaya hizo kutatua matatizo mbalimbali kama vile elimu, afya na maji na utawalenga wazee, watoto na miradi ya kuongeza kipato kwa wenye uwezo wa kufanya kazi.

Akizungumzia uzinduzi huo, Mwamanga alisema baadhi ya kaya masikini zilizofaidika katika mradi wa majaribio watatoa ushuhuda.

Vile vile akasema “hafla hiyo itatoa fursa kwa Serikali kuweka bayana dhamira yake ya kupanua na kuwafikia wananchi wengi zaidi” kwenye mpango wa kukabiliana na uamsikini.

Akizungumzia awamu ya pili ya Tasaf, Mwamanga alisema pamoja na kuonyesha mafanikio, changamoto kubwa ilikuwa ni uwezo mdogo wa kifedha wa kutekeleza miradi yote iliyobuniwa na wananchi.

“Miradi iliyopangwa kutekelezwa ilikuwa 5,950 (sawa na asilimia 10) wakati maombi kutoka kwa wananchi yalifikia 102,275,” alisema Mwamanga.

Akizungumzia juu ya namna kaya masikini zitakavyopatikana katika awamu ya tatu, Mtaalamu wa Utafiti na Ushirikishwaji wa Mambo ya Kijamii wa Tasaf, Amedeus Kamagenge alisema watatumia mikutano mikuu ya kijiji na mitaa.

Vile vile vigezo sahihi, akaeleza kuwa vitatambuliwa baada ya sifa za wahusika kuchambuliwa na kompyuta zenye programu maalumu za kuchambua mifumo ya umasikini.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo