Ikiwa usiku wa kuamkia hii leo
zoezi la sensa ya watu na makazi limeanza kutekelezwa nchi nzima, wilayani
Makete zoezi hilo limeanza kwa amani na utulivu kama ilivyotarajiwa huku mkuu wa wilaya hiyo akiwa wa
kwanza kuhesabiwa
Akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kuhesabiwa, mkuu wa wilaya ya Makete ambaye pia ni
mwenyekiti wa kamati ya sensa wilaya Bi Josephine Matiro amewataka wananachi
kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani wa sensa
Amesema maswali yanayoulizwa ni
mepesi na yanayojibika hivyo haoni sababu ya wananchi wake kuogopa kuzungumza
ama kutoa taarifa kwani kila kitu kipo wazi na haichukui muda mrefu
“Unajua watu wengi wanakuwa na
hofu, mimi naona hizo hofu hazina maana kwanza maswali yenyewe ni marahisi,
hayaumizi kichwa na wala hayapotezi muda, cha masingi makarani wa sensa
wakifika kwako wewe kama mkuu wa kaya ni kutoa taarifa tuu, kama nlivyofanya
mimi kwa kuwa nami nimeshahesabiwa muda mchache uliopita na namshukuru Mungu
kuwa wa kwanza hii leo kuhesabiwa”alisema
Amesema zoezi la sensa ya watu na
makazi haliathiri utendaji kazi wa shughuli za wananchi na kuwataka wananchi
kutoacha kufanya shughuli zao kutokana na kusubiri kuhesabiwa
Pia ameitaka jamii kusaidia
kuonesha maeneo tete ambayo watu huwepo ikiwemo waliopo misituni kupasua mbao,
ama waliopo maporini kuchoma tofali, ili makarani wa sensa wawafuate huko
waliko na taarifa zao ziweze kuchukuliwa na makarani wa sensa
Matiro amewataka wakuu wa kaya
kutayarisha ipasavyo taarifa za watu wote waliolala kwenye kaya yake usiku wa
kuamkia leo, ili aweze kuzitoa kwa makarani wa sensa pindi watakapofika kwenye
kaya zao kuendesha zoezi la sensa
Zoezi la sensa ya watu na makazi
linaendelea kutekelezwa nchi nzima likiongozwa na kauli mbiu isemayo SENSA KWA
MAENDELEO JIANDAE KUHESABIWA na litaendeshwa kwa siku saba mfululizo hivyo
wananchi mnaombwa kutoa ushirikiano
