JUMLA ya Maduka ya dawa za kilimo na Mifugo 40 kutoka katika wilaya za
Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi yamefungwa kutokana na makosa
mbalimbali yakiwemo ya kukosa vibali, kuuza dawa bandia, dawa
zilizopitwa na wakati na kusababisha wakulima na wafugaji kupata
hasara kubwa baada ya mazao na mifugo yao kuathiriwa.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msajili wa viwatilifu nchini Dr.Bakari Kaoneka amesema taasisi hiyo imeimarisha ukaguzi nchini kote baada ya kukithiri kwa udanganyifu kutoka kwa wafanyabiashara na
kusababisha kero kubwa.
Amesema zoezi hilo ni la kudumu na litaendelea kwa mikoa mingine yote
ili kuwabaini wauzaji wa dawa za mifugo na kilimo bandia na zile zilizopitwa na wakati ili kuwanususru wakulima na wafugaji ambao wengi
wao wamekuwa wakipata hasara baada ya kununua dawa hizo.
Amesema kuwa awali walikutana na upinzani mkubwa na kulazimika kutumia nguvu kuyafunga maduka hayo baada ya wafanyabiashara hao kukaidi amri ya kufunga maduka yao baada ya kuwapatia amri ya kuyafunga.
Aidha wapo baadhi ya wafanyabiashara waliunga mkono zoezi hilo kwa
madai kuwa ni kuleta uimara na ufanisi katika kupunguza hasara zisizo
za lazima kwa wakulima,wafugaji na hata wafanyabiashara wenyewe.
