Arusha,
Kuna uwezekano kwamba vitambulisho vya kitaifa
walivyonavyo
raia wa Afrika Mashariki vinaweza siku moja kutumika kama hati mbadala
ya
kusafiria ndani ya kanda hiyo, iwapo hatua iliyoanzishwa na Kenya na
Rwanda
itaenezwa katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Nchi nyingine wanachama wa EAC ni pamoja na
Tanzania,Uganda
na Burundi.
“Kenya tayari ina mipango ambayo iko mbioni kuingia
katika
makubaliano na Rwanda kuruhusu raia wa nchi mbili hizo kuwa huru kuvuka
mipaka
kati yao kwa kutumia vitabulisho vya utaifa wao,” alisema Mwenyekiti wa
Baraza
la Mawaziri wa Afrika Mashariki, Musa Sirma.
Sirma, ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano Afrika
Mashariki
wa Kenya aliongeza kuwa nchi hizo mbili pia zitabadilishana maafisa wa
uhamiaji
kutoa huduma kwenye kaunta za mataifa yao.
“Huo ndio mwanzo wa kuyafanya mataifa yote matano
ya EAC
kuondoa mahitaji ya hati za kusafiria miongoni mwa raia wake kama
walivyoweza
kuondoa viza kwa wasafiri wa ndani ya kanda ,” Sirma alibainisha.
Waziri aliyasema hayo mjini Kigali,Rwanda katika
mkutano wa
Tano wa Vyombo vya Habari vya Afrika Mashariki uliandaliwa na
Sekretarieti ya
EAC kwa kushirikiana na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki kwa
kuungwa
mkono na Trade-Mark East Africa.
Kenya na Rwanda tayari zimeshatoa vitambulisho
vyake vya
taifa ambapo Tanzania inaendelea na mchakato wa kufanya hivyo huku
hakuna
harakati zozote za aina hiyo kwa nchi za Uganda na Burundi.
Robert Mugabe, ambaye ni Mhariri Mkuu wa Chapisho
la ‘Great
Lakes’ Voice,’ ambaye hana uhusiano na Rais wa Zimbabwe, alisema hati za
kusafiria ni ghali kwa raia wa Afrika Mashariki kwa sababu nchini Rwanda
inawagharimu sawa na dola za Kimarekani 100 (zaidi ya shilingi
150,000/-).
“Ninafurahi sana kusikia kuwa hivi karibuni itakuwa
bure
kwenda Kenya kuliko ilivyokuwa huko nyuma nilipompeleka mama yangu kwa
matibabu
na kulazimika kulipia hati yake ya kusafiria kwa dola za Kimarekani
mbali na
gharama za matibabu,” Mugabe alisema na kuongeza kuwa ilikuwa ni vigumu
hata
kwa waandishi wa habari waliohitaji kuvuka mipaka mara kwa mara.
EAC imekuwa ikitoa hati za kusafiria za jumuiya
hiyo ambayo
mbali na kutumika kwa kusafiria kwa wanachama wa mataifa hayo
iliwahakikishia
wamiliki wake kipindi cha kubaki nchi wanayotembelea kwa miezi sita
lakini
kuondolewa hivi karibuni kwa viza miongoni mwa nchi wanachama wa EAC
imepelekea
kutokutumika kwake kwa sasa.
Mwandishi Mkongwe Jenerali Ulimwengu kutoka
Tanzania hapo
awali aliipongeza serikali ya Rwanda kwa kufungua milango kwa raia
kutoka
mataifa mengine manne ya EAC wanaotaka kufanya kazi au kuishi nchini
humo kama
wangependa kufanya hivyo.
Wakati huohuo, ilibainika pia katika mkutano huo
kuwa
ufufuaji wa reli ya Afrika Mashariki ni ufumbuzi pekee wa kupambana na
vikwazo
vinavyoathiri mwingiliano wa kibiashara ndani ya nchi wanachama wa
jumuiya
hiyo.