HATARI YA MAKETE KUKUMBWA NA MLIPUKO WA MAGONJWA IKIWEMO KIPINDUPINDU




 Mji wa Makete
Ikiwa zimepita siku tatu baada ya mkurugenzi mtendaji wa halmshauri ya wilaya ya Makete Imelda Ishuza kufanya mkutano na wafanyabiashara wa soko kuu la Makete mjini na kuwataka kuchukua hatua za haraka za kutengeneza choo cha soko hilo, hatimaye uongozi wa soko hilo umeanza kuchukua hatua za awali za kutatua kero hiyo

Akizungumza na wanahabari sokoni hapo katibu wa soko hilo Bw. Asifiwe Luvanda amesema kufuatia mkutano walioufanya na mkurugenzi Agosti 17 mwaka huu, waliagizwa kutengeneza mara moja choo hicho kwani kimejaa, hivyo wameanza kutekeleza agizo hilo

Amesema hatua ambayo wameichukua hadi sasa ni kupeleka taarifa hizo kwa Bwana Afya wa wilaya Boniphace Sanga kuona kama watatakiwa kutengeneza choo kipya ama kuna namna ambayo itaweza kutumiwa, ili choo hicho kiendelee kutumika

Amesema ushirikiano ndio unahitajika zaidi kutoka kwa wafanyabiashara wote, idara ya afya wilaya ya Makete pamoja na wadau mbalimbali ili kutatua kero hiyo

“Unajua mimi nina wasiwasi sana kama tutafanikiwa katika hili ingawa sisi kama viongozi inabidi tutekeleze agizo la mkurugenzi, lakini nina wasiwasi na ushirikiano kutoka kwa wafanyabiashara wenzangu”alisema Luvanda

Waandishi wa habari waliofika eneo hilo wameshuhudia choo hicho kikiwa kimejaa na pia ipo hatari ya kutokea mlipuko wa magonjwa kama vile kipindupindu muda wowote kuanzia sasa kwa kuwa bado wafanyabiashara hao wanaendelea kujisaidia katika choo hicho ingawa kimejaa

Hadi mwandishi wetu anaandika habari hii juhudi za kumpata bwana afya wilaya ya Makete Boniphace Sanga kuhakikisha kama taarifa hizo zimeshafikishwa ofisini kwake zimegonga mwamba mara baada ya simu yake kutopatikana

Agosti 17 mwaka huu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya makete alifanya mkutano na wafanyabiashara hao ambapo pamoja na mambo mengine aliwaagiza viongozi hao kutatua kero ya choo ambacho kimejaa

Na Riziki Manfred


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo