DC MAKETE AFUNGUA MAFUNZO YA SENSA NGAZI YA WILAYA HII LEO



DC MAKETE MH. JOSEPHINE MATIRO AKIFUNGUA MAFUNZO HAYO
MRATIBU WA SENSA MAKETE BI NURU MWENDAPOLE AKIZUNGUMZA NA WASHIRIKI
DODOSO REFU LA SENSA 2012

Na Edwin Moshi, Makete

Makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi wilayani Makete wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza zoezi hilo kwa umakini kama serikali ilivyowaagiza ili malengo ya zoezi hilo yafanikiwe

Akifungua mafunzo kwa makarani na wasimamizi hao wa sensa wilayani Makete hii leo, Mwenekiti wa kamati ya sensa wilayaya ya Makete ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo Mh. Josephine Matiro amesema dhamana waliyopewa ni kubwa na itatekelezwa na wao katika wilaya hiyo hivyo wanatakiwa kufuata mafunzo wanayopatiwa kwani ni njia pekee ya kufanikisha zoezi hilo

Amesema pamoja na mambo mengine wanamafunzo hao wanatakiwa kutunza usiri mkubwa wa taarifa za sensa ambazo watazikusanya kwa watu pamoja na kuuliza maswali kadri ya uwezo wao ili waweze kuelewa namna watakavyokwenda kutekeleza zoezi hilo

Mh. Matiro ameeleza pia mandalizi ya sensa kwa wilaya ya Makete yamekamilika na mengine yanaendelea kutekelezwa kwani maandalisi mengine yanahitaji utekelezaji wake kwa jinsi siku zinavyozidi kwenda

“Ndugu zangu naomba niwatoe hofu, serikali ipo makini na maandalizi hapa wilayani yamekamilika hivyo tunaomba msituangushe, mmepewa dhamana kubwa ya kutekeleza zoezi la sensa ngazi ya wilaya, mpo waalimu tena ambao mnaaminika kuliko watu wengine, lakini pia na wote mliochaguliwa kufanya zoezi hili nawaombeni mlifanikishe ipasavyo” alisema Matiro

Ameongeza kuwa kazi ya uhamasishaji ngazi ya wilaya inaendelea kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizopo wilayani hapo, ikiwemo redio, matangazo kwa uma, mikutano ya hadhara, makanisani, misikitini, mabango na vipeperushi mbalimbali, hivyo wananchi wengi wanauelewa wa kutosha kuhusu sensa

Awali akimkaribisha mkuu wa wilaya, mratibu wa sensa ngazi ya wilaya Bi. Nuru Mwendapole amesema jumla ya washiriki 484 wilaya nzima wanapatiwa mafunzo hayo wakiwemo wadadisi wa dodoso refu wapatao 430, wasimamizi 32 pamoja na wadadisi wa ziada wapatao 22, na wote hao wanapatiwa mafunzo katika vituo vine tofauti ambavyo ni Iwawa, Tandala, Bulongwa na Matamba

Mkuu huyo wa wilaya pamoja na wajumbe wa kamati ya sensa wilaya mbali na kushiriki katika ufunguzi wa mafunzo hayo pia walishiriki wakati wa mafunzo na kujionea jinsi washiriki walivyokuwa wakipatiwa mafunzo ya utekelezaji wa zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo