DC ATAKA WAZAZI KUFUATILIA MAENDELEO YA WATOTO WAO SHULENI


MKUU wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu amewataka wazazi wa wanafunzi wa shule za msingi za Tarafa ya Amani Wilayani hapa kuwa na ada ya kufuatilia maendeleo ya watoto wao mashuleni pamoja na kupiga vita mimba za utotoni.

Akizungumza kwa nyakati tofauti juzi katika vijiji mbalimbali vya Tarafa ya Amani wakati wa uhamasishaji wa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi, Mgalu alisema kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakijisahau umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

Alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya msingi hadi ya sekondari bure na hivyo ni wazazi kufuatilia maendeleo ya mtoto wao lengo likiwa ni kupata elimu stahiki ambayo itamsaidia katika maisha yake ya baadae.

Alisema kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwashirikisha watoto wao katika kazi za kijamii pamoja na kilimo wakati wa masomo jambo ambalo linachangia kwa kiwango kikubwa kumfanya mtoto kutopenda shule.

“Ndugu zangu wa Tarafa ya Amani na vitongoji vyake muliopo hapa kunisikiliza, nimepata taarifa kuwa huku kuna tatizo la utoro wa wanafunzi na mimba shuleni, hivyo natoa onyo kuwa nimekuja kimapambano” alisema Mgalu

Mgalu alisema amekuja katika Wilaya hiyo kushirikiana na wananchi wa Muheza katika suala zima la maendeleo ikiwa na pamoja na kuleta umoja na mshikamano katika jamii huku akiwa na taarifa za kukithiri kwa mimba mashuleni jambo ambalo amedai atalivalia njuga.

Alisema suala hilo limekuwa likimuumiza kichwa na kumnyima usingizi na kuahidi kulifuatilia ili kukomesha vitendo hivyo na moja ya mbinu ambazo atazitumia ni kuitisha vikao vya wazazi na walimu na kupanga mikakati ili kuhakikisha mimba na utoro mashule unatokomea.

Alisema chanzo cha watoto kubeba mimba utotoni na kuacha masomo shuleni inasababishwa na wazazi majumbani ikiwa na pamoja na malezi hivyo ni vyema kuitisha vikao vya walimu na wazazi na kuweza kujadili namna ya kuweza kuondosha tatizo hilo.

Alisema ikiwa wazazi watakuwa na ushirikiano mzuri na walimu ikiwa na pamoja na wanafuzi wao tatizo la mimba na utoro mashuleni linaweza kuondoka na kuifanya Wilaya hiyo kufanya viruri katika ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo